Buenos Aires, Argentina
Lionel Messi amewaaga kiaina mashabiki Argentina akifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Venezuela, mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyopigwa kwenye dimba la Monumental mjini Buenos Aires.
Akionekana mwenye sura iliyojaa bashasha, Nessi ambaye hiyo inatajwa kuwa huenda ndiyo mechi yake ya mwisho ya ushindani kwenye ardhi ya kwao Argentina, alisema hilo ni tukio alilokuwa akiliota kwa muda mrefu sasa.
Messi, 38, akiwa ameambatana na watoto wake watatu, mbele ya mashabiki wapatao 80,000 waliokuwa uwanjani hapo, mashabiki hao walimpa heshima kwa kusimama na kumsalimia kabla ya mechi hiyo kuanza.
Mchezaji huyo mwenye rekodi ya kushinda tuzo za Ballon d’Or mara nane, ndiye aliyekuwa nahodha wakati Argentina ikibeba Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mwaka 2022 na hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 114 katika mechi 194.
“Kuna mengi ya kuvutia niliyopitia, ni mengi katika soka, lakini wakati wote huwa ni furaha kucheza soka Argentina mbele ya watu wetu, nina furaha sana kumaliza jambo hili hapa, ni kitu nilichokuwa nikikiota wakati wote,” alisema Messi.
Messi alisema kwa miaka mingi amekuwa akifurahia ya mazuri ya Barcelona, na ndoto yake imekuwa ni kuyapata hayo kwao Argentina, nchi yake na mbele ya watu wake licha ya kuwa mengi yamekuwa yakisemwa lakini ameachagua kubaki na yale yote mazuri.
Argentina ambayo inaongoza kundi lake katika mbio za kufuzu Kombe la Dunia ikiwa tayari imefuzu, mabao yake matatu ya ushindi katika mechi na Venezuela, mbali na mawili ya Messi, bao jingine lilifungwa na Lautaro Martinez.
Kuhusu hatma ya Messi kama ataendelea kuichezea Argentina au ndio ameanza kuaga, licha ya uvumi wa kustaafu kwake kuibuka mara kwa mara lakini mwenyewe amesema bado hajaamua lolote hadi sasa ikiwamo kama atacheza fainali za Kombe la Dunia au la.
“Najitahidi niwe vizuri lakini zaidi ya yote niwe mkweli kwa nafsi yangu, nikijiona nipo vizuri nafurahia hilo lakini ikiwa kinyume chake ukweli ni kwamba sitokuwa na furaha kwa hiyo nitachagua kuondoka,” alisema Messi.
