Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetoka sare ya bao 1-1 na timu ya Congo Brazaville katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 wakati Morocco ikiwa timu ya kwanza kufuzu kwa nchi za Afrika.
Katika mechi ya Stars iliyochezwa Ijumaa hii usiku, Septemba 5, 2025, kwenye dimba la Alphonce Masamba, wenyeji Brazaville ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 68 lililofungwa na Mousavaou.
Mfungaji wa bao hilo alipiga shuti ambalo halikuwa kali lakini lilimshinda mlinda mlango wa Stars, Yakoub Syleiman na kuibua shangwe kwa mashabiki wa Congo.
Juhudi za Stars kusaka bao la kusawazisha zilizaa matunda katika dakika ya 84 kwa bao lililofungwa na Ramadhan Mwalim, mchezaji ambaye aliingia akitokea benchi akichukua nafasi ya Clement Mzize na kuongeza kasi ya mashambulizi kwa Stars.
Mwalimu alifunga bao hilo baada ya kuinasa pasi ya nahodha Mbwana Samatta na kuambaa na mpira kabla ya kupiga shuti la chini chini lililomshinda kipa wa Congo, Chelcy Bonazebi.
Timu hizo ziliuanza mchezo kwa kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 21, Samatta aliangushwa na beki mmoja wa Congo wakati akianza kuipangua safu ya ulinzi na mwamuzi kuamuru upigwe mpira wa adhabu ambao Samatta aliupiga lakini ulidakwa na kipa Bonazebi.
Dakika chache baada ya bao la Stars, Congo waliiwashia moto Stars wakisaka bao la pili lakini Deogracias Bassinga alishindwa kuitumia vizuri pasi ya Mignon Koto kwa kupiga shuti lililotoka nje akiwa karibu na lango la Stars.
Kwa matokeo hayo Stars sasa imefikisha pointi 10 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara Morocco na Jumanne ijayo itacheza na Niger na kumalizia mechi ya mwisho dhidi ya Zambia ambayo itachezwa mwezi ujao.
Iwapo Stars itashinda mechi hizo mbili itakuwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwa kuwa moja ya timu nne zitakazocheza play offs baada ya kila kundi kutoa timu moja itakayofuzu moja kwa moja fainali hizo.
Kwa upande wa Congo timu hiyo ni kama imeshaziaga mbio hizo hasa baada ya kuathiriwa na adhabu ya kufungiwa kwa shirikisho la soka la nchi hiyo na ingawa adhabu hiyo ilifutwa mwezi Mei, hadi sasa timu hiyo ina pointi moja tu.
Moroco yafuzu Kombe la Dunia 2026
Katika mechi nyingine ya kuwania kufuzu, Morocco au Atlas Lions imefuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Niger mabao 5-0, ushindi uliopatikana kwenye uwanja mpya wa Moulay Abdellah mjini Rabat, uwanja ambao ndio kwanza umezinduliwa.
Mabao ya Morocco katika mechi hiyo yalifungwa na Ismael Saibari aliyefunga mawili, la kwanza katika dakika ya 29 kwa krosi ya Eliesse Ben Seghir na la pili dakika 10 baadaye akiitumia pasi ya Achraf Hakimi.

Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Ayoub El Kaabi dakika ya 51, Hamza Igamane dakika ya 69 na la mwisho lilifungwa na Azzedine Ounahi dakika ya 84.
Katika mechi hiyo mambo yalianza kuwaharibikia Niger katika dakika ya 26 walipalazimika kucheza 10 uwanjani baada ya Abdoul-Latif Goumey kulimwa kadi nyekundu na dakika tatu baada ya tukio hilo, Niger walijikuta wakipachikwa bao la kwanza.
Kwa ushindi huo, Morocco watakuwa na furaha mara mbili katika siku za hivi karibuni baada ya kubeba taji la michuano ya Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2025 hivi karibuni katika michuano iliyofanyika, Tanzania, Kenya na Uganda.
