Leverkusen, Ujerumani
Aliyekuwa kocha wa Man United, Erik ten Hag amefutwa kazi na klabu ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi mbili za Ligi Kuu Ujerumani yaani Bundesliga.
Ten Hag alikabidhiwa majukumu ya kuinoa Leverkusen majira ya kiangazi msimu huu baada ya kutimuliwa Man United Oktoba mwaka jana akiwa ameinoa timu hiyo kwa miaka miwili na nusu.
Ten Hag aliulaumu uongozi wa Leverkusen kwa kutompa muda na nafasi ya kuifanyia kazi dira ya klabu na kufafanua kuwa kutimuliwa kwake si jambo sahihi na limeonesha kuwa hakukuwa na mahusiano mazuri na ya kuaminiana.
Kutimuliwa kwa Ten Han kunafanya idadi ya makocha wa zamani wa Man United kupoteza kazi zao kufikia watatu baada ya Ole Gunnar Solskjaer kutimuliwa na klabu ya Besiktas na Jose Mourinho naye kutimuliwa katika klabu Fenerbahce.
“Uamuzi wa Bayer Leverkusen kuniondoa katika kazi hakika ni jambo la kushangaza, kuachana na kocha baada ya mechi mbili tu za ligi si sahihi,” alisema Ten Hag.
Ten Hag alisema wakati wa majira ya kiangazi wachezaji wengi waliokuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo waliondoka na hivyo kazi ya kuijenga timu mpya inahitaji umakini, muda pamoja na kuaminiana.
Kocha huyo pia alisema aliianza kazi ya kuinoa timu ya Leverkusen kwa kujituma na nguvu zote lakini bahati mbaya uongozi haukuwa tayari kumpa nafasi ya kuifanyia kazi dira ya yao, kuweka viwango na kutengeneza staili ya uchezaji.
