Fenerbahce, Uturuki
Kocha Jose Mourinho ametimuliwa katika klabu ya Fenerbahce ya Uturuki baada ya kuinoa katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja.
Kutimuliwa kwa Mourinho kumekuja siku chache baada ya timu hiyo kutolewa na Benfica kwenye mechi za play-off za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika taarifa ya kumfuta kazi kocha huyo, klabu ya Fenerbahce ilimshukuru Mourinho kwa juhudi zake na kumtakia kila la heri.
Mourinho, 62, ni kati ya makocha wenye jina kubwa barani Ulaya akiwa hadi sasa amezinoa timu za FC Porto, Chelsea, Man United, Tottenham, Inter Milan, Real Madrid na AS Roma.
Katika msimu uliopita, Mourinho aliiwezesha Fenerbahce kumaliza Ligi Kuu Uturuki akiwa nafasi ya pili lakini mara kadhaa alijikuta katika matukio yaliyojaa utata.
Februari mwaka huu, vinara wa ligi kuu nchini Uturuki, Galatasaray walitangaza nia ya kumfungulia kesi ya jinai kwa madai ya kutoa kauli za ubaguzi wa rangi baada ya timu hizo mbili kutoka sare ya bila kufunga.
Mourinho hata hivyo aliigeuzia kibao klabu hiyo akikana madai hayo na kusisitiza kwamba yeye ni mtu anayechukia ubaguzi wa rangi na badala yake akawafungulia mashtaka akitaka Galatasaray wamlipe fidia ya Euro 41,000 kwa kumharibia jina.
Katika mechi ya Europa Ligi dhidi ya United, mechi iliyochezwa Oktoba mwaka jana na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Mourinho alisema baada ya kuachana na Fenerbahce atainoa timu iliyo chini ya msimamo wa ligi ili asipate nafasi ya kushiriki michuano ya Uefa.
Nchini Uturuki, Mourinho aliwahi kufungiwa mechi nne ingawa baadaye zilipunguzwa na kuwa mbili baada ya kutoa kauli ya kulalamikia ubora wa waamuzi mara baada ya mechi yao dhidi ya Galatasaray.
Sambamba na mataji ya ligi za ndani barani Ulaya, Mourinho pia ana rekodi ya kubeba taji la ligi ya mabingwa mara mbili, kwanza na FC Porto na baadaye akiwa Inter Milan.
Kimataifa Mourinho atimuliwa Fenerbahce
Mourinho atimuliwa Fenerbahce
Read also
