Kampala, Uganda
Matumaini ya timu ya taifa ya Uganda ‘Uganda Cranes’ kufuzu nuzu fainali ya michuano ya Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 yametoweka baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Senegal.
Uganda, timu pekee mwenyeji wa michuano hiyo iliyobaki nayo ilishindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani na hivyo kutolewa kama ilivyokuwa kwa majirani zake wa Kenya na Tanzania.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii Agosti 23, 2025 kwenye Uwanja wa Namboole, Senegal, ambao ni mabingwa watetezi waliandika bao hilo pekee dakika ya 62 lililofungwa na Oumar Ba.
Oumar Ba alifunga bao hilo akiwa ndani ya eneo la 18 kwa mpira uliomshinda kipa Joel Mutakubwa na kuwanyamazisha maelfu ya mashabiki waliofurika kwenye uwanja huo wakiwa na matumaini ya timu yao kusonga mbele.
Michuano hiyo inayofanyika katika nchi za Kenya Uganda na Tanzania ilianza kutimua vumbi Agosti 2 na itafikia tamati Agosti 30 kwa mechi ya fainali huku nchi hizo tatu wenyeji zikibaki kuwa mashuhuda.
Mechi za nusu fainali zitachezwa Jumanne Agosti 26, 2025 kati ya Madagascar dhidi ya Sudan kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na nusu fainali nyingine Morocco itaumana na Senegal kwenye Uwanja wa Namboole.
Washindi wa mechi hizo wataumana katika mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Kasarani mjini Nairobi, mechi ambayo itamtangaza bingwa mpya wa CHAN 2024.
Kimataifa Uganda Cranes yatolewa CHAN
Uganda Cranes yatolewa CHAN
Read also
