London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta ameingiwa hofu baada ya winga wake Bukayo Saka kuuumia katika mechi dhidi ya Leeds iliyopigwa Jumamosi, Agosti 23, 2025, mechi ambayo Arsenal ilishinda kwa mabao 5-0.
Saka ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya England, ndiye aliyeifungia Arsenal bao la pili lakini mambo yaliharibika kipindi cha pili baada ya kwenda chini akionesha dalili za kuwa na maumivu.
Tukio hilo lilitokea kipindi cha pili ambapo Saka bila ya kuzongwa na mchezaji wa timu pinzani alikwenda chini na hapo hapo akatolewa na nafasi yake kuingia Leandro Trossard.
Kuumia kwa Saka kuliibua huzuni zaidi kwani hapo kabla nahodha wa timu hiyo, Martin Odegaard naye alilazimika kutoka uwanjani katika kipindi cha kwanza baada ya kuumia bega.
Furaha pekee waliyoipata mashabiki wa Arsenal ni kukamilika kwa usajili wa Eberechi Eze kutoka Crystal Palace ambaye kabla ya mechi hiyo alitangazwa kujiunga na Arsenal kwa ada ya Pauni 67.5 milioni.
Kinachomtesa Arteta kwa Saka ni ukweli kwamba mchezaji huyo msimu uliopita alikuwa nje ya uwanja kwa takriban miezi minne akiwa majeruhi wa misuli jambo ambalo limemtokea kwa mara nyingine.
“Bukayo, akiwa anakimbia na mpira, ameumiliki mpira, akiwa anamkabili beki alijisikia kitu kinamuuma, kwa hiyo ngoja tuone, nafikiri ni matatizo ya misuli, si mguu ule ule wa awali,” alisema.
Arteta aliongeza kuwa kitendo cha Saka kutoka nje ni wazi kwamba tatizo litakuwa kubwa na kuhusu Odegaard alisema mchezaji huyo atahitaji kufanyiwa ‘scan’.
