Na mwandishi wetu
Timu za Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania, zimetolewa katika michuano ya Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024.
Harambee imetolewa na Madagascar katika robo fainali baada ya kulala kwa penalti 4-3 wakati Taifa Stars nayo ikitolewa katika hatua hiyo hiyo na Morocco kwa kufungwa bao 1=0.
Mechi zote za timu hizo zimechezwa Ijumaa hii Agosti 22, 2025, Harambee ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kasarani, Nairobi na Taifa Stars ikiwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya Taifa Stars, timu hizo zilipambana katika dakika 45 za kwanza bila kufungana hadi dakika ya 65 Morocco walipopata bao hilo pekee lililofungwa na Oussama Lamlaoui.
Lamlaoui ambaye hadi sasa ana mabao matatu alifunga bao hilo baada ya kuinasa pasi ya Youssef Belammari kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa wa Taifa Stars, Yakoub Suleiman.

Taifa Stars ambao waliingia uwanjani wakitambia rekodi ya kutopoteza hata mchezo mmoja hadi kufuzu robo fainali, walicheza kwa kujiamini wakishambulia lango la Morocco mara kadhaa lakini Morocco wakati wote walionesha utulivu na umakini.
Morocco nao walifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini ukuta wa Taifa Stars ulikuwa mgumu hasa kipa Yakoub ambaye mara kadhaa alifanya kazi ya ziada kuokoa mashambulizi.
Nao Harambee Stars mambo yao hayakuwa mazuri mbele ya Madagascar baada ya kutolewa kwa penalti katika mechi ambayo hadi dakika 90 za kawaida na zile za nyongeza zinamalizika timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.

Ikiwa mbele ya maelfu ya mashabiki kwenye dimba la Kasarani, Harambee ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 63 lililofungwa na Alphonce Omija aliyeruka juu kuuwahi mpira na kuujaza wavuni kwa kichwa.
Bao hilo liliibua kelele za furaha kwa mashabiki wa Harambee waliojazana kwenye dimba la Kasarani wakijiaminisha kuwa timu yao ilikuwa katika hatua nzuri ya kufuzu nusu fainali.
Utulivu wa Madagascar ulizaa matunda dakika ya 70 baada ya timu hiyo kupata penalti iliyotolewa baada ya Lewis Bandi kuunawa mpira uliopigwa na Toky Randriamirindra.
Madagascar hatimaye walifufua matumaini kupitia penalti hiyo baada ya Fenohasina Razafimaharo kuujaza mpira wavuni akimchambua kipa wa Harambee, Bryne Omondi na kuipatia Madagascar njia ya kuelekea kwenye mikwaju ya fainali tano tano.
Katika mikwaju ya penalti, kipa wa Madagascar, Ramandimbisoa Lalainiranjaka aliokoa penalti moja wakati Omondi wa Harambee naye aliokoa penalti moja huku penalti ya Alphonce Omija ikienda nje ya lango na hivyo kuipa Madagascar ushindi wa 4-3.

Michuano ya CHAN 2024 ilianza kutimua vumbi Agosti 2 mwaka huu huku wenyeji wakiwa ni nchi majirani Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda ikitarajiwa kufikia tamati kwa mechi ya fainali itakayopigwa Jumamosi, Agosti 30, 2025.
Kushindwa kwa Harambee na Taifa Stars kunawafanya wenyeji hao kuaga mashindano hayo katika hatua ya robo fainali na kubaki mashuhuda wa michuano hiyo.
Uganda Cranes ndiyo timu pekee mwenyeji iliyosalia katika michuano hiyo na Jumamosi, Agosti 23, 2025 wataumana na Senegal katika mechi nyingine ya robo fainali.
