Mallorca, Hispania
Hatimaye Marcus Rashford amecheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Hispania au La Liga akiwa na timu yake mpya ya Barcelona ambayo anaichezea kwa mkopo akitokea Man United.
Rashford amecheza mechi hiyo ya kwanza ya ushindani Jumamosi hii Agosti 16, 2025 dhidi ya Mallorca, mechi ambayo Barcelona au Barca imetoka na ushindi wa mabao 3-0.
Mabao ya Barca katika mechi hiyo yamefungwa na Raphinha dakika ya saba akiitumia krosi ya Lamine Yamal wakati bao la pili lilifungwa na Ferran Tores dakika ya 23 na la mwisho lilifungwa na Yamal dakika za lala salama.
Mechi hiyo hata hivyo ilikuwa ngumu mno kwa Mallorca ambao walijikuta wakicheza tisa uwanjani baada ya wachezaji wake Manu Morlanes na Vedat Muriqi kupewa kadi nyekundu.
Morlanes alipewa kadi ya kwanza ya njano kwa kuchelewesha muda kabla ya kupewa kadi ya pili kwa kumchezea rafu Yamal.
Muriqi alipewa kadi kwa rafu dhidi ya kipa mpya wa Barca, Joan Garcia, awali mchezaji huyo alipewa kadi ya njano lakini baada ya mwamuzi kuliangalia tukio hilo kupitia VAR aliamua kumpa kadi nyekundu moja kwa moja.
Kwa upande wa Rashford aliingia uwanjani dakika ya 69 akitokea benchi na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza kutoka England kucheza mechi ya ushindani ya La Liga baada ya Gary Lineker kufanya hivyo mwaka 1989.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye hapo kabla alizungumzia matamanio yake ya kuichezea Barca, alicheza nafasi ya mshambuliaji wa kati lakini hakuweza kupata bao.
Usajili wa Rashford na nyota mwingine mpya wa timu hiyo, Garcia ulikamilika asubuhi ya kabla ya mechi kwa sababu ya matatizo ya kanuni za matumizi ya fedha yaliyokuwa yakiikabili Barca.
Kimataifa Rashford acheza mechi ya kwanza La Liga
Rashford acheza mechi ya kwanza La Liga
Read also
