Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski amebainisha kuwa alitamani kusaini na klabu ya Manchester United mwaka 2012 ili kufanya kazi na kocha wa wakati huo, Sir Alex Ferguson.
Mpango wa mchezaji huyo kujiunga na timu hiyo ya Old Trafford hata hivyo haukuweza kufanikiwa baada ya klabu yake ya wakati huo, Borussia Dortmund kuzuia usajili huo.
Lewandowski hata hivyo alibaki Ujerumani baada ya kusajiliwa na klabu ya Bayern Munich mwaka 2014 akiwa mchezaji huru.
“Kuhusu kwenda Manchester United niliamua na kusema sawa, nilitaka kujiunga na Manchester United ili kuonana na Alex Ferguson,” alisema.
Lewandowski alifafanua kuwa licha ya kuikubali Man United, Dortmund walikataa kumuuza kwa sababu walifahamu kama angebaki pengine wangeweza kupata pesa zaidi na hivyo alitakiwa kusubiri labda kwa mwaka mmoja au miwili.
Wakati mchezaji huyo akitamani kwenda Man United, Dortmund ilikuwa ikinolewa na kocha Jurgen Klopp ambaye baadaye alihamia Liverpool na kujipatia mafanikio.
Lewandowski ambaye pia aliwahi kutakiwa na klabu ya Blackburn Rovers pia ya England kwa sasa ana fikra tofauti kuhusu kushindwa kwake kucheza soka katika Ligi Kuu England.
“Labda ni jambo la kujuta kwa kutocheza katika Ligi Kuu England lakini nikiangalia huko nilipotoka hadi kucheza Bayern Munich, Dortmund na sasa Barcelona nalazimika kusema kwamba nina furaha katika maisha yangu ya soka,” alisema.
Kimataifa Lewandowski aliitamani Man United
Lewandowski aliitamani Man United
Read also
