London, England
Kocha wa zamani wa Man United, Erik Ten Hag amesema aliyekuwa mchezaji wake katika timu hiyo, Cristiano Ronaldo hakuwahi kuwa tatizo wakati wake akiwa kocha.
Ronaldo aliyetamba Man United kwa miaka mingi kabla ya kurejea mara ya pili mwaka 2021, alionekana kutokuwa na maelewano mazuri na Ten Hag hadi akaamua kundoka baada ya mwaka mmoja.
Ten Hag naye alitimuliwa Oktoba mwaka jana akiwa katika siku zake za mwanzo mwanzo za msimu wa 2024-25 kutokana na mwenendo usiopendeza wa timu hiyo na kocha huyo baadaye akajiunga na Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Akizungumza Ijumaa Agosti 8, 2025 baada ya mechi ya kirafiki kati ya Leverkusen na Chelsea, mechi iliyopigwa Stamford Bridge na Chelsea kushinda kwa mabao 2-0, Ten Hag alisema kwa yeye Ronaldo hakuwahi kuwa tatizo ingawa jambo hilo limepita.
Uhusiano duni kati ya Ronaldo na Ten Hag ulikuwa gumzo na kumulikwa na vyombo vya habari kwa kipindi ambacho winga huyo kutoka Ureno alikuwa na timu hiyo.
“Nafikiri ilikuwa kama ilivyokuwa, ni mambo yaliyopita na baada ya hapo tulishinda mataji mawili na Manchester United, namtakia kila la kheri kwa mambo yake ya baadaye na namtakia yote yaliyo mazuri,” alisema Ten Hag.
Ten Hag ambaye mbele ya wengi alionekana kufeli akiwa Man United lakini hadi anaondoka aliiwezesha timu hiyo kubeba mataji mawili, la Carabao mwaka 2023 pamoja na lile la FA mwaka 2024.
Kitendo cha kocha huyo kubeba taji la FA kiliwashangaza wengi kwa kuwa alishinda kwa kuwabwaga mahasimu wao Man City ambao walikuwa vinara na tishio kwenye Ligi Kuu England.
Ten Hag hata hivyo hakutaka kuzungumza kwa sana kuhusu Ronaldo badala yake alisisitiza kuwa anapenda kushinda mataji na ndilo jambo ambalo amekuwa akilifanya kwa maisha yake yote ya soka na anataka kuendelea na hilo na ndiyo changamoto aliyonayo wakati huu akiwa kocha wa Leverkusen.
