Manchester, England
Hatimaye klabu ya Manchester United imekamilisha usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wa RB Leipzig ya Ujerumani, Benjamin Sesko kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 73.8 milioni.
Sesko ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Slovenia, amekuwa akihusishwa na timu hiyo katika siku za karibuni na amesaini mkataba wa miaka mitano.
Usajili wa Sesko unaifanya idadi ya wachezaji wa kuimarisha safu ya ushambuliajii waliosajiliwa Man United kufikia watatu, kabla yake walisajiliwa Matheus Cunha na Bryan Mbeumo.
Sesko ambaye ndio kwanza ana miaka 22, pia alikuwa akiwindwa na Newcastle United lakini ni Man United waliofanikiwa kumsajili na sasa mchezaji huyo atakuwa chini ya kocha Ruben Amorim.
Man United inapambana kuimarisha kikosi baada ya mambo kwenda kombo msimu uliopita kwa kumaliza ligi ikiwa nafsi ya 15 na hivyo kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya klabu barani Ulaya.
“Ni jambo lililo wazi kwamba historia ya Manchester United ni ya kipekee, lakini kitu kinachonivutia ni mambo yajayo, tulipojadili mpango huu ilikuwa wazi kwamba kila kitu kipo sawa katika timu hii kwa ajili ya kuendelea kukua na kupigania mataji kwa mara nyingine,” alisema Sseko.
Sesko pia alisema baada ya kuwasili katika klabu hiyo aliiona nguvu ya ushindi na mazingira ya kifamilia yaliyotengenezwa hivyo anaamini Man United ni mahala sahihi kwake kufikia kiwango chake cha juu na kukamilisha matamanio yake yote.
Aliongeza kuwa anasubiri kwa hamu kuanza kujifunza kutoka kwa Ruben (kocha) na kuungana na wachezaji wenzake wa Man United kwa lengo la kufanikisha mafanikio ambayo wote wanajua kwamba wana uwezo wa kufanya hivyo.
Sesko alijiunga na Leipzig mwaka 2023 na hadi anaondoka ameacha rekodi ya mabao 39 katika mechi 87 za mashindano yote.
