Los Angeles, Marekani
Klabu ya soka ya Los Angeles (LAFC) ya Marekani imetangaza kukamilisha usajili wa mchezaji mkongwe wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Korea Kusini, Son Heung-Min.
Habari zinadai kuwa usajili wa mchezaji huyo umeigharimu klabu hiyo zaidi ya dola 25 milioni na hivyo kuvunja rekodi ya Atlanta United FC iliyomsajili mshambuliaji Emmanuel Lette Lath kwa dola 22 milioni.
Kwa kukamilisha usajili huo, Son sasa anakuwa amehama kwenye Ligi Kuu England na kujiunga na Ligi Kuu Marekani au MLS, moja ya ligi za soka duniani zinazopata umaarufu siku hadi siku.
Mkataba wa Son na Spurs unafikia ukomo katika Majira ya Kiangazi mwaka 2026 lakini mkataba wake na Los Angeles FC unafikia ukomo mwaka 2927 lakini ana fursa ya kuuongeza hadi mwaka 2029.
Akizungumzia kujiunga kwake na timu hiyo, Son alisema kwamba anajivunia kujiunga na klabu yenye matamanio makubwa na kuhamia katika moja ya miji mikubwa duniani iliyobobea katika michezo.
“Los Angeles ni mji uliojaa historia ya mabingwa, nipo hapa kuandika ukurasa mwingine, nimeifurahia hii changamoto mpya MLS, nimekuja Los Angeles kubeba mataji na kujitolea kwa klabu, jiji hili na mashabiki, nasubiri kwa hamu kuanza kwa msimu,” alisema Son.
Mara ya mwisho Son aliichezea Spurs katika mechi ya kirafiki dhidi ya Newcastle, mechi ambayo ilichezwa kwao Korea Kusini, Jumapili iliyopita.
Siku moja baada ya mechi hiyo, Son akiwa katika hali ya unyonge alitangaza nia yake ya kuachana na Spurs, timu aliyoichezea miaka 10 kwa mafanikio.
