Na mwandishi wetu
Bao pekee la Shomari Kapombe limeiwezesha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kutoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritanni katika mechi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano hii Agosti 6, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Stars ilipata wakati mgumu kuipenya ngombe ya Mauritania kabla ya kupata bao hilo pekee dakika ya 89.
Mpira uliozaa bao la Stars ulianzia kwa kiungo Shekham Ibrahim aliyepiga pasi ndefu iliyotua kwa Idd Suleiman ‘Nado’ ambaye aliutuliza vizuri mpira kabla ya kupiga pasi nyingine ndefu iliyomkuta Kapombe aliyeujaza mpira wavuni.
Kocha wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliwapongeza wachezaji wake kwa namna ambavyo walionesha upambanaji hadi kuivunja ngombe ngumu ya Mauritania.
Kwa ushindi huo Stars sasa inakuwa imefikisha pointi sita katika Kundi B baada ya ushindi wa awali wa mabao 2-0 mbele ya Burkina Faso na hivyo kuwa kinara wa kundi hilo ambalo pia lina timu za Afrika ya Kati na Madagascar.
Burkina Faso ambayo iliilaza Afrika ya Kati mabao 4-2 katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa awali, sasa inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu.
Stars itajitupa tena uwanjani Jumamosi, Agosti 9, 2025 kuikabili Madagascar, mechi ambayo ushindi utaihakikishia timu hiyo tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Kimataifa Stars yailaza Mauritania 1-0
Stars yailaza Mauritania 1-0
Read also
