Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Man United aliyeuzwa kwa mkopo Barcelona, Marcus Rashford amesema anaamini timu hiyo itatafuta pesa za kukamilisha usajili wake moja kwa moja.
Rashford alijiunga na Barcelona au Barca mwezi uliopita akitokea Man United lakini bado hajasajiliwa La Liga sababu ikiwa ni hali ya kifedha ya klabu yake hiyo mpya.
Zikiwa zimebakia wiki mbili kabla ya pazia la La Liga kufunguliwa ambapo Barca itaanza kwa kuumana na Mallorca, Rashford hana wasiwasi na mazingira anayopitia kwa sasa.
Sambamba na Rashford, Barca pia inahitaji kukamilisha usajili wa La Liga kwa wachezaji wengine ambao ni Gerard Martin, Joan GarcÃa, Roony Bardghji na Wojciech Szczesny.
Akizungumzia hilo, rais wa klabu hiyo, Joan Laporta aliwahakikishia mashabiki wake kwamba hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa klabu inalifanyia kazi suala hilo.
Kwa upande wake Rashford alisema klabu inalifanyia kazi suala lake na anaamini kila kitu kitakuwa sawa na kwa sasa anachofanya ni kuwa makini mazoezini na kujiandaa na msimu mpya wakati huu timu hiyo ikiwa imeweka kambi nchini Korea Kusini.
“Tuko tayari kwa ajili ya kuanza msimu mpya,, maandalizi ya msimu yanakwenda vizuri, ni jambo zuri kuwa sehemu ya timu, nafurahia kuzoeleka kwenye timu, namzoea kocha,” alisema Rashford.
Rashford alisema anaamini timu hiyo itafanya makubwa zaidi kuliko msimu uliopita na alipoulizwa atapenda kumaliza msimu akiwa amefunga mabao mangapi, mchezaji huyo alicheka na kujibu 100.
