Nairobi, Kenya
Rais wa Kenya, William Ruto ameahidi kutoa kitita cha Sh milioni 600 za Kenya zaidi ya Sh 11.5 bilioni za Tanzania kwa wachezaji wa timu ya soka ya nchi hiyo, Harambee Stars.
Kiongozi huyo ameahidi kuwapa wachezaji hao fedha hizo iwapo watafanikiwa kubeba taji la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2024).
Sambamba na ahadi hizo, Rais Ruto pia alisema atawapa wachezaji hao Sh 60 milioni (TSh 1.2 bilioni) iwapo watafikia hatua ya robo fainali na Sh 70 milioni (TSh 1.4 bilioni) kama watafikia hatua ya nusu fainali.
Kama ahadi hiyo haitoshi, rais huyo wa Kenya pia aliahidi kutoa kitita cha Sh milioni 90 (TSh 1.8 bilioni) iwapo wachezaji hao watafanikiwa kufikia hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Harambe Stars ambao wamepangwa Kundi A katika michuano hiyo lenye timu za Moroco, DR Congo na Zambia, watatupa karata yao ya kwanza Jumapili hii dhidi ya DR Congo.
Zawadi za Rais Ruto pia zitatolewa kwa kila mechi ambayo wachezaji hao watashinda ambapo kila mchezaji atapewa Sh milioni moja (TSh 19.5 milioni) na iwapo watatoka sare kila mchezaji atapewa Sh 500,000 (TSh 9.7 bilioni).
Rais Ruto alitoa ahadi hizo wakati akipata chai na wachezaji hao Jumamosi hii asubuhi katika Hoteli ya Pullman mjini Nairobi.
Michuano ya CHAN ambayo itachezwa kwa kipindi cha mwezi mmoja inafanyika katika nchi tatu majirani wa Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania, imeanza rasmi Jumamosi hii Agosti 2, 2025 jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Katika salamu zake kwa Wakenya, Rais Ruto alimtaka kila raia wa nchi hiyo kuifanya Harambee Stars kuwa chama chake cha siasa na kwenda na kauli mbiu ya Stars Must Win yaani Stars lazima ishinde.
Kimataifa Rais awapa ahadi nono Harambee Stars
Rais awapa ahadi nono Harambee Stars
Read also
