Chicago, Marekani
Kocha wa Man United, Ruben Amorim ameweka wazi kuwa msimu uliopita alikuwa akisafiri kwenda kucheza mechi huku akiwa mwenye hofu ya matokeo kwa timu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika ziara ya timu hiyo nchini Marekani, kocha huyo amekiri kuwa msimu uliopita wa 2024-25 ulikuwa mgumu kwake.
Katika msimu huo, Man United ilimaliza ligi katika nafasi ya 15, ni nafasi mbaya kuwahi kuishika ambayo mara ya mwisho kuwa katika nafasi kama hiyo ilikuwa msimu wa 1989-90.
Amorim ambaye alikabidhiwa jukumu la kuinoa Man United Novemba 2024, baada ya Erik ten Hag kutimuliwa, ameiongoza timu hiyo kushinda mechi saba kati ya 27 na kupoteza mechi ya fainali ya Europa Ligi mbele ya Tottenham.
Alipoulizwa alikuwa akijisikiaje mbele ya familia yake kila baada ya kufungwa mechi mfululizo, Amorim alisema kipindi kigumu na kilichokuwa kikimtatiza zaidi ni vikao vya maandalizi ya mechi.
“Niwaambie ukweli kipindi kigumu haikuwa pale ninaporudi nyumbani baada ya mechi badala yake ni hali ya kufikiria namna ya kumkabili mpinzani, kwa sababu kuna wakati niliona mapema kwamba tutakuwa na wakati mgumu,” alisema Amorim.
Alisema mapambano yote na ugumu waliokuwa wakikutana nao alianza kuhisi yote hayo kabla ya mechi na hicho ndicho kipindi kilichokuwa kigumu mno kwake.
Amorim hata hivyo alisema kwamba kwa sasa hajikuti katika hali hiyo ngumu na bado hajawa mwenye kufurahia kazi yake lakini anaamini kuna siku nzuri mbele yake.
Katika uongozi wake, Amorim aliteua wachezaji sita wakiongozwa na Bruno Fernandes, Tom Heaton, Noussair Mazraoui, Harry Maguire, Diogo Dalot na Lisandro Martinez kwa ajili ya kusimamia ubora na mambo madogo madogo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
