Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imetozwa faini ya Sh milioni tatu kwa makosa ya kwenda kinyume na taratibu wakati wa mechi dhidi ya mahasimu wao, Yanga iliyopigwa Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Taarifa ya TFF iliyopatikana Alhamisi Julai 17, 2025 iliyataja makosa hayo kuwa ni kushindwa kuhudhuria mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi jambo ambalo ni la lazima.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, adhabu ya kosa hilo ni Sh milioni moja wakati kosa la pili ni kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo huo ambapo faini yake pia ni Sh milioni moja.
Simba ambao katika mechi hiyo walifungwa mabao 2-0, kosa lao la tatu ni kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, kosa ambalo adhabu yake pia ni faini ya Sh milioni moja.
Simba imepewa adhabu hiyo baada ya kikao cha kamati ya uendeshaji na usimamizi cha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kupitia mwenendo wa matukio mbalimbali ya ligi ya msimu wa 2024-25 uliomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kamati hiyo pia imeipa onyo timu ya Ken Gold kwa kuchelewa kuingia uwanjani wakati wa mechi yao na Simba iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Timu ya Tabora United nayo imetozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kutohudhuria mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi yao na Azam FC.
Fountain Gate nayo imetozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kulazimisha kupita kwenye eneo lililowekwa uzio wakati wa mchezo wao wa play-off dhidi ya Stand United.
Stand United nayo imetozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la mashabiki wao kumrushia mawe mwamuzi msaidizi namba moja katika mchezo wao na Fountain Gate uliopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nao wachezaji Edgar Williams wa Fountain Gate na Seleman Richard wa Stand United kila mmoja amefungiwa michezo mitatu na faini ya Sh 500,000 kwa kukataa kuingia vyumbani wakati wa mapumziko, wachezaji hao walibaki uwanjani kila mmoja akimtegea mwenzake aingie kwanza.
Soka Simba yapigwa faini ya Sh milioni tatu
Simba yapigwa faini ya Sh milioni tatu
Read also
