London, England
Arsenal imekamilisha usajili wa winga, Noni Madueke kutoka klabu ya Chelsea kwa ada ya Pauni 48.5 milioni.
Usajili wa Madueke umeonekana kushangaza kwani mchezaji huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Chelsea waliokuwa na timu hiyo nchini Marekani kwenye fainali za michuano ya Fifa ya Klabu ya Dunia.
Madueke, 23, hata hivyo aliondoka kwenye kambi ya Chelsea kabla ya timu hiyo kucheza mechi ya fainali dhidi ya PSG iliyopigwa Jumapili na Chelsea kutoka na ushindi wa 3-0 na kubeba taji la michuano hiyo.
Arsenal imempa Madueke mkataba wa miaka mitano ambao ada yake kwa ujumla pamoja na malipo mengine inaweza kufikia Pauni 50 milioni.
“Nimefurahi na najiona mwenye baraka kuwa hapa, ahsanteni kwenu wote mliofanikisha mimi kuwa hapa, nasubiri kwa hamu kuingia uwanjani na kuanza kulipa imani mliyonionesha, litakuwa jambo la kipekee,” alisema Madueke.
Madueke alijiunga na Chelsea Januari 2023 akitokea PSV Eindhoven kwa ada ya Pauni 30 milioni na hadi anaondoka ameichezea timu hiyo maea 92 na kufunga mabao 20.
Kabla ya kujiunga na PSV aliyodumu nayo miaka minne na nusu, Madueke ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Enland, alianza kucheza katika akademi za Crystal Palace na baadaye Tottenham.
Madueke amezoeleka kucheza katika wingi ya kulia ambayo amezoeleka kucheza Bukayo Saka ingawa pia anamudu wingi ya kushoto.
