
Barcelona, Hispania
Winga wa Barcelona, Lamine Yamal amewahi kukataa kufananishwa kwa vyovyote na Lionel Messi lakini sasa amelazimika kubebeshwa hadhi hiyo baada ya kukabidhiwa rasmi jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na mchezaji huyo.
Klabu ya Barcelona au Barca imethibitisha hilo Jumatano hii, Julai 16, 2025 ikiwa ni siku tatu zimepita baada ya winga huyo kusherehekee miaka 18 tangu kuzaliwa kwake.
Yamal ataanza rasmi kuvaa jezi namba 10 mwanzoni mwa msimu mpya wa 2025-26 na kabla yake jezi hiyo ilikuwa ikivaliwa na Ansu Fati ambaye mapema mwezi huu alikamilisha taratibu za kujiunga na Monaco kwa mkopo.
Fati alikabidhiwa jezi namba 10 mwaka 2021 kutoka kwa Messi lakini tangu wakati huo amekuwa akiandamwa na janga la kuwa majeruhi na kushindwa kuwa na namba ya uhakika kwenye kikosi cha kwanza.
Tukio la kumkabidhi Yamal jezi namba 10 lilishuhudiwa na familia yake na kuunganishwa na hafla ya mchezaji huyo kupewa mkataba mpya ambao unafikia ukomo mwaka 2031.
“Nilipokuwa mtoto ndoto yangu ilikuwa kucheza kwa mara ya kwanza Barca, kukua na kucheza nikiwa na jezi namba 10, kila mtoto aliyezaliwa Barcelona ana ndoto hiyo, Messi amefanya yake, nami nitafanya yangu,” alisema Yamal.
Kabla ya hapo, Yamal alikuwa akivaa jezi namba 19 na kitendo cha kumkabidhi jezi yenye namba ya Messi kinamuacha mchezaji huyo katika mtihani wa kusaka mafanikio kama ya Messi.

Messi alianza kuivaa jezi namba 10 akiwa na Barca mwaka 2008 na hadi anaondoka mwaka 2021 na kujiunga na PSG, amefanikiwa kuacha alama ya kipekee ya mafanikio.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kubeba mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, 10 ya La Liga, tuzo mbalimbali binafsi na rekodi ya kuwa mfungaji bora kinara wa wakati wote wa klabu hiyo.
