Madrid, Hispania
Kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti amenusurika kwenda jela mwaka mmoja baada ya kukutwa na hatia katika kosa la ukwelpaji kodi lakini ametakiwa kulipa faini.
Ancelotti ambaye pia amewahi kuzinoa timu za Everton, Chelsea na Real Madrid alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kukwepa kulipa kodi inayofikia Pauni 830,000.
Fedha hizo zinadaiwa kutokana na mshahara wake katika kipindi chake cha kwanza akiwa na timu ya Real Madrid kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 na badala ya kwenda jela ametakiwa kulipa faini ya Pauni 333,100.
Ancelotti, 66 aliachana na Real Madrid mwishoni mwa msimu ulioisha wa 2024-25 na kukabidhiwa jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Brazil inayowania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa sheria za Hispania, adhabu yoyote ya chini ya miaka miwili ambayo haitokani na kosa la ukatili wa kijinai ni mara chache sana kumfanya mtuhumiwa afungwe jela hasa pale inapotokea amekutwa na kosa hilo kwa mara ya kwanza.
Mapema mwaka huu wakati akitoa ushahidi wake, Ancelotti aliiambia mahakama kwamba hakuwahi hata kuwaza kama alikuwa akifanya kosa la ukwepaji kodi.
Badala yake alisema kwamba alipopewa mshahara wa jumla wa Pauni milioni 5.1 na klabu ya Real Madrid, alilikabidhi suala hilo kwa washauri wake wa masuala ya fedha.
Wengine waliowahi kutozwa faini kwa kukwepa kodi nchini Hispania ni mchezaji wa zamani wa Barcelona, Lionel Messi mwaka 2017 alihukumiwa kwenda jela miezi 21, baadaye adhabu ilipunguzwa na akatozwa faini ya Pauni 230,000.
Cristiano Ronaldo naye mwaka 2019 alilazimika kulipa faini ya Pauni 17.5 milioni kwa kukwepa kodi wakati akiwa Real Madrid.
Kocha Jose Mourinho naye wakati akiinoa Real Madrid kati ya mwaka 2011-12 alitozwa faini ya Pauni milioni 2.1.
Kimataifa Ancelotti anusurika kwenda jela
Ancelotti anusurika kwenda jela
Read also
