Katika mkakati wa kusaka mafanikio kwa msimu mpya wa 2025-26, Azam FC ya Tanzania imemtangaza rasmi, Florent Ibenge (pichani kulia) kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Tukio hilo limekuja baada ya kuwapo habari kwa siku za karibuni kuhusu kocha huyo mwenye heshima yake barani Afrika kujiunga na Azam na hatimaye Jumamosi ya Julai 5, 2025, timu hiyo imemtangaza rasmi.
Ibenge, 63, kocha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) amejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Al Hilal Omdurman ya nchini Sudan.
Ujio wa Ibenge unatajwa kuwa mwanzo mpya kwa Azam ambayo licha ya uwekezaji mkubwa lakini kwa muda mrefu sasa imekuwa ikihaha kusaka mafanikio ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa rasmi, Ibenge alisema anaijua ligi ya Tanzania kuwa ni yenye ushindani huku akiutaja uhasama uliopo baina ya timu za Yanga na Simba.
“Tunajua kwamba Yanga na Simba ni timu kubwa lakini pia sisi tunayo hadhi na dhamira ya kushindana, niko hapa kwa ajili ya kushinda na kuipeleka hii klabu mahali inapotakiwa kuwa,” alisema Ibenge.
Ibenge si jina geni katika soka la Afrika kwani mbali na kuzinoa klabu kadhaa maarufu pia amewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya DR Congo.
Miongoni mwa mafanikio ya Ibenge ni pamoja na kuiwezesha timu ya taifa ya DR Congo kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2015.
Katika klabu, Ibenge aliiwezesha AS Vita kufikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014 na mwaka 2022 akiwa na RS Berkane ya Morocco aliiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika.
