Lyon, Ufaransa
Klabu maarufu Ufaransa ya Olympique Lyonnais au Lyon imeshushwa daraja hadi Ligi 2 baada ya ukaguzi wa mahesabu uliofanywa katika klabu hiyo na Taasisi ya Ukaguzi wa Fedha kwa Klabu za soka Ufaransaya (DNCG).
Lyon ambao wamewahi kuwa mabingwa mara saba wa Ligi Kuu Ufaransa au Ligi 1 hata hivyo wametangaza kukata rufaa haraka kupinga uamuzi huo.
Uamuzi wa kuishusha daraja timu hiyo awali ulifikiwa Novemba mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ukata na mahesabu ya timu kuwa hovyo kabla ya uamuzi huo kuthibitishwa hivi karibuni.
Katika kupinga uamuzi wa DNCG, klabu hiyo ilitoa taarifa ikieleza kuwa imefanya kila ilichoweza kukidhi matakwa ya taasisi hiyo ya kifedha.
Katika taarifa hiyo klabu ya Lyon ilieleza kutambua uamuzi uliofikiwa na DNCG na kuthibitisha kuwa watakata rufaa haraka iwezekanavyo.
“Kwa namna ambavyo tumeweka wazi mambo yetu ya kifedha na mafanikio ya kimichezo ambayo klabu imeyapata hadi kushiriki ligi Ulaya kwa miaka miwili hakika tunashindwa kuelewa ni vipi uongozi unachukua maamuzi ya kuishusha daraja klabu hii kubwa Ufaransa,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
Uamuzi wa kuishusha daraja Lyon umefikiwa ikiwa ni siku chache baada ya mfanyabiashara maarufu nchini Marekani, Textor kuamua kuuza asilimia 43 ya hisa zake katika klabu ya Crystal Palace ya England.
“Tunashukuru mchango wa wanahisa wetu, na kuuzwa kwa Crystal Palace, uwezo wetu kifedha umekuwa mkubwa, na sasa tuna rasilimali za kutosha kwa ajili ya msimu wa 2025-26,” ilifafanua taarifa ya Lyon.
Oktoba mwaka jana zilikuwapo habari kuwa kampuni ya Eagle Football Group, inayomilikiwa na Textor ina madeni yanayofikia Pauni milioni 422 hali iliyoibua hofu kuhusu uimara wa kifedha wa klabu ya Lyon.
Baada ya taarifa hiyo, Lyon ilianza kuuza wachezaji kadhaa akiwamo Rayan Cherki ambaye alijiunga na Manchester City.
Kimataifa Lyon yashushwa daraja Ufaransa
Lyon yashushwa daraja Ufaransa
Read also
