Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeachana na kiungo Fabrice Ngoma na hivyo mchezaji huyo hatokuwa na timu hiyo kwenye Ligi Kuu NBC na michuano ya kimataifa kwa msimu ujao wa 2025-26.
Kuachwa kwa mchezaji huyo kumewekwa wazi kupitia vyanzo mbalimbali vya habari nchini Tanzania mojawapo ikiwa ni kauli ya mchezaji huyo kuwaaga mashabiki wa timu hiyo.
Inaelezwa kuwa mkataba wake umefikia ukomo na uongozi hauna nia ya kumuongezea mkataba mpya lakini hadi sasa haijaelezwa wazi ni kwa nini Simba imeachana na nyota huyo kutoka DR Congo.
Uwajibikaji wake katika timu ni kati ya mambo yasiyotia shaka, uwezo wake pia unatosha kumfanya aendelee kuwa na Simba kwa lengo la kuipa mafanikio zaidi timu hiyo katika msimu mpya.
Msimu wa 2024-25, Simba imeishia nafasi ya pili Ligi Kuu NBC lakini imeweka rekodi ya kipekee kwa kufika hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika, michuano ya klabu inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mara ya mwisho Simba kufikia hatua ya fainali ya michuano ya klabu inayoandaliwa na CAF ilikuwa mwaka 1993, wakati mwaka huu ilishindwa kutamba mbele ya RS Berkane ya Morocco, mwaka 1993 Simba ilishindwa kutamba mbele ya Stellah ya Ivory Coast.
Kutowekwa wazi kwa sababu hasa za kuachwa kwa Ngoma imekuwa chanzo cha mawazo yasiyo rasmi kuibuka kutoka kwa wadau wa soka nchini wakiwamo mashabiki wa Simba na hata mahasimu wao Yanga.
Wapo wanaolalamikia hatua hiyo wakidai kwamba si sahini kwa kuwa Ngoma alihitajika kuendeleza mafanikio ya Simba kwa kpiga hatua zaidi ya walipoishia msimu wa 2024-25.
Hapo hapo kuna ambao tayari wanamhusisha mchezaji huyo na matukio ya kudai posho katika namna isiyo sahihi, wengine wanamhusisha na mzozo wake na kipa Mousa Camara katika moja ya mechi za Simba na je amepata ulaji sehemu nyingine? yote haya ni mambo yanayojadiliwa.
Mwisho wa yote uongozi wa Simba kwa msaada wa benchi la ufundi ndio wanaojua sababu hasa ya kufikia uamuzi huo, kwa sasa tumtakie kila la kheri Ngoma huko aendako.
Kimataifa Kwa nini Fabrice Ngoma?
Kwa nini Fabrice Ngoma?
Read also
