Florida, Marekani
Beki wa kati wa Real Madrid, David Alaba (pichani) amepata matatizo ya misuli na huenda akakosa kuiwakilisha timu yake kwenye michuano ya Fifa ya Klabu ya Dunia inayoendelea nchini Marekani.
Habari kuhusu matatizo ya Alaba zimethibitishwa na klabu hiyo Ijumaa hii na imeelezwa kuwa beki huyo mkongwe mwenye miaka 33 ataanza kwa kuikosa mechi ya Jumanne dhidi ya Juventus.
Matatizo ya beki huyo ni mwendelezo wa majanga yanayomuandama kwani tayari alishazikosa mechi tatu za michuano hiyo wakati akiuguza maumivu ya goti la kushoto aliyoyapata mwezi Aprili.
Kama mambo yatakwenda vizuri baada ya mechi hiyo ya Jumanne, Real Madrid itacheza mechi ya robo fainali Julai 5 na kufuatiwa na nusu fainali Julai 9 na fainali Julai 13.
“David anachukua muda mrefu kidogo, baada ya kufanyiwa operesheni tunahitaji kuwa makini na wenye kusubiri, hatua moja hadi nyingine, tutasubiri zaidi,” alisema kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso.
Katika michuano hiyo ya Fifa, Real Madrid inashiriki bila ya wachezaji wake tegemeo wa kikosi cha kwanza ambao ni Eder Militao, Dani Carvajal na Eduardo Camavinga ambao wanaendelea na mazoezi ya kujiweka fiti.
Wachezaji wengine ambao ni majeruhi ambao pia inaelezwa wanatarajiwa kupona na kurudi uwanjani ni Ferland Mendy na Endrick ambao kwa sasa wapo Madrid wakipambana kujiweka fiti.
Akiwazungumzia wachezaji hao, Alonso hata hivyo alisema Ferland bado ana muda mrefu hadi kupona wakati matumaini makubwa ya kupona na kuwa fiti yapo kwa Eduardo.
