Na mwandishi wetu
Mwamuzi Amin Mohammed Omar (pichani) kutoka Misri ndiye atakayekuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi ya mahasimu wa soka Tanzania, Yanga na Simba, itakayochezwa Jumatano, Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Uteuzi wa mwamuzi huyo wa kigeni umekuja baada ya kuwapo mjadala kuhusu nani mwamuzi sahihi wa kuchezesha mechi hiyo ambayo mshindi wake atakabidhiwa taji la Ligi Kuu NBC msimu wa 2024-25.
Mbali na mwamuzi huyo wengine watakaomsaidia ambao pia wanatokea Misri ni Mahmoud Ahmed na Samir Gamal wakati mwamuzi msaidizi atakuwa Ahmed Mahrous na kamisaa wa mchezo huo atakuwa Salim Singano ambaye anatokea Tanga.
Kabla ya waamuzi hao kutangazwa majina kadhaa ya waamuzi wakiwamo Ahmed Arajiga, Ramadhan Kayoko, Kefa Kayombo na wengineo yamekuwa yakijadiliwa katika siku za karibuni hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Hatimaye TFF wamekuja na uamuzi tofauti kwa kuwakabidhi mechi hiyo waamuzi kutoka Misri ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya mechi hiyo maarufu Dar Derby kuchezeshwa na waamuzi kutoka taifa hilo.
Yanga wanamkumbuka mwamuzi Omar kwa kuwa ndiye aliyekuwa mwamuzi katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mechi iliyopigwa Machi mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamina Mkapa na kumalizika kwa sare ya 0-0.
Simba nao wanamkumbuha mwamuzi huyo katika mechi yao ya Ligi ya Mabngwa Afrika dhidi ya Horoya ya Guinea, iliyopigwa Februari 2023 nchini Guinea na Simba kulala kwa bao 1-0.
Mechi ya Simba na Yanga itachezwa baada ya kuahirishwa mara mbili kufuatia mivutano iliyojitokeza, awali ilikuwa ichezwe Machi 8, 2025 lakini ukaibuka mvutano baada ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi.
Kitendo hicho kiliwafanya viongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuiahirisha kwa sababu walizozitaja kuwa ni za kiusalama huku Simba wakidai kwamba wasingecheza mechi siku hiyo hadi waliowazuia kufanya mazoezi watakapoadhibiwa.
Baadaye TPLB walitangaza kuahirisha mechi hiyo kwa sababu kadhaa kubwa ikiwa ni ya kiusalama na ndipo Yanga nao walipoibuka wakisema hawako tayari kucheza siku nyingine hadi waliohusika kuahirishwa kwa mechi hiyo watakapoadhibiwa.
TPLB walitangaza mechi hiyo ingechezwa Juni 15, 2025 kabla ya kuahirishwa kwa mara nyingine na kutangaza tarehe ya sasa ambayo ni Juni 25 na waamuzi kutoka Misri kupewa majukumu.
Yanga wameonesha utayari wa kucheza mechi hiyo wakati Simba wakionekana kutoonesha msimamo wao kama watacheza au hawatacheza badala yake wamekuwa wakitoa madai kwamba mamlaka za soka zinaibeba Yanga.
Kimataifa Waamuzi wa Misri wapewa mechi ya Simba, Yanga
Waamuzi wa Misri wapewa mechi ya Simba, Yanga
Read also
