Manchestern, England
Mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford ameelezea shauku yake ya kutaka siku moja acheze kwenye timu moja na mshambuliaji nyota wa Barcelona, Lamine Yamal (pichani).
Rashford, 27, amekuwa nje ya kikosi cha Man United kuanzia nusu ya msimu uliopita wa 2024-25 baada ya kuuzwa kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa.
Man United iliamua kumtoa Rashford baada ya mshambuliaji huyo kutokuwa na namba ya uhakika kikosi cha kwanza na zipo habari kwamba klabu hiyo sasa inasikilizia ofa kwa timu yoyote itakayomtaka wakati wowote kuanzia sasa.
Zimewahi kuwapo habari kwamba mchezaji huyo anatakiwa na klabu za Inter Milan, PSG, Barcelona, Juventus na hata Bayern Munich.
Akizungumza hivi karibuni kuhusu uwezekano wa kucheza kikosi kimoja na Yamal, Rashford alisema ndio na kufafanua kuwa kila mtu duniani anapenda kucheza na aliye bora.
Yamal licha ya kuwa na umri mdogo wa miaka 17 lakini ametokea kuwa mmoja wa wachezaji mahiri duniani na mchango wake umeonekana kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania iliyobeba taji la Ulaya (Euro 2024) pamoja na Barcelona iliyobeba taji la La Liga msimu ulioisha hivi karibuni wa 2024-25.
“Ni vigumu kuzungumza kwa maneno kuhusu kile anachokifanya, hakutakiwa kufanya hicho wakati akiwa na miaka 16 na 17,” alisema Rashford.
Kwa sasa Rashford anasubiri kurudi Man United na kuanza rasmi mazoezi kujiandaa na msimu mpya wa 2025-26 kama mipango ya kuhama itagonga mwamba lakini akiwa Villa ameifungia timu hiyo mabao manne katika mechi 17 na tayari amerudishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England na kocha Thomas Tuchel.
