Na waandishi wetu
Timu za Yanga na Simba zimeendeleza moto kwenye Ligi Kuu NBC kwa kupata ushindi wa mabao 5-0 kila moja, Yanga ikiichapa Prisons na Simba ikitoa kipigo kama hicho kwa Ken Gold.
Ushindi wa timu hizo umepatikana leo Jumatano Juni 18, 2025 zikiwa zimebaki siku takriban sita kabla ya timu hizo mahasimu wa soka Tanzania kukutana kwenye mechi nyingine ya ligi hiyo.
Matokeo ya mechi za leo yanazidi kuongeza ushindani katika kuwania taji la ligi hiyo msimu huu wa 2024-25 ambao unaelekea ukingoni huku Yanga ikishika usukani na pointi 76 katika mechi 28 na Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 75 katika mechi 28.
Simba ikiwa kwenye dimba la Ali Hassan mwinyi mjini Tabora ilianza kuziona nyavu za wapinzani wao dakika ya 20 kwa bao la Kibu Denis kabla ya Elly Mpanzu kuongeza la pili dakika mbili baadaye.
Nyota ya Kibu ambaye alikuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, iliendelea kung’ara dakika ya 25 alipopachika bao la tatu na Jean Ahoua kufunga la nne na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 4-0.
Bao la tano na la mwisho kwa Simba lilipatikana dakika ya 76 mfungaji akiwa Jean Ahoua, bao ambalo linamfanya kiungo huyo kuzidi kung’ara katika orodha ya wafungaji wenye mabao mengi ya ligi akiwa amefikisha 16.
Kwa upande wa Yanga wakiwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya waliandika bao lao la kwanza kupitia kwa Mudathir Yahya kabla ya Clatous CHama kuandika la pili wakati mabao mengine matatu yalifungwa na Israel Mwenda na Pacome Zouzoua aliyefunga mawili.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, matokeo ni kama ifuatavyo…
Azam FC 5-0 Tabora United
Coastal Union 1-0 Fountain Gate
Singida BS 2-1 Dodoma Jiji
Pamba 1-0 JKT Tanzania
Mashujaa 1-1 KMC
Namungo 0-0 Kagera Sugar
