Florida, Marekani
Kiungo mpya wa Man City, Tijjani Reijnders (pichani) amesema hajajiunga na timu hiyo kwa lengo la kuziba pengo la Kevin De Bruyne ambaye ameihama City na hapo hapo Reijnders akasajiliwa.
Reijnders amekiri kuwa De Bruyne ni kati ya wachezaji waliokuwa wakimvutia, amejiunga na Man City kwa ada ya Pauni 46.5 milioni akitokea Ac Milan lakini ameipinga hoja kwamba yuko Man City kuziba pengo la mchezaji huyo.
De Bruyne ameachana na Man City baada ya kuichezea timu hiyo kwa miaka 10 ambapo Reijnders amekiri kuwa alivutiwa na soka la kiungo huyo pamoja na Andres Iniesta wa Barcelona na Hispania.
Reijnders alisema akiwa Man City atajaribu kuwa yeye na si De Bruyne kwani hajajiunga na timu hiyo kwa lengo la kuziba pengo la kiungo huyo mkongwe wa Ubelgiji.
“Siko hapa kuchukua nafasi yake, lazima nicheze soka langu lakini huwa nachukua vitu kwa wachezaji tofauti pamoja na mazuri wanayoyafanya na kuyaiga yakiwamo ya De Bruyne kwa namna alivyokuwa akiusoma mchezo na kutoa pasi,” alisema Reijnders.
De Bruyne alitamba Man City chini ya kocha Pep Guardiola na aliwahi kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa Ligi Kuu England mara mbili na hatua yake ya kuhama timu hiyo na kusajiliwa Reijnders ilitafsiriwa kwamba City imesajili mbadala wa De Bruyne.
Reijnders, 26, yupo nchini Marekani na Man City kwenye michuano ya Fifa ya Klabu ya Dunia na amekuwa akitajwa miongoni mwa viungo bora wa Serie A huku akipewa nadasi kubwa ya kutamba katika timu hiyo mpya.
Reijnders pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uholanzi ambayo alianza kuichezea mara ya kwanza mwaka 2023 na hadi sasa ameichezea mara 23 na kuifungia mabao manne.
