Na mwandishi wetu
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Almas Kasongo (pichani) amesimamishwa kazi wakati mwenyekiti wa bodi hiyo, Steven Mnguto ametangaza kujiuzulu.
Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyopatikana leo Juammosi, Juni 14, 2025 imeeleza kuwa Mnguto amewasilisha TFF barua ya kujiuzulu nafasi yake.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau hata hivyo haikuwekwa wazi sababu hasa za Mnguto kuamua kujiuzulu nafasi yake.
Kuhusu Kasongo, taarifa hiyo pia haikuweka wazi sababu hasa za TFF kuchukua uamuzi huo badala yake ilielezwa kwa kifupi kuwa Rais wa TFF, Walace Karia ndiye aliyechukua uamuzi wa kumsimamisha kiongozi huyo.
Wakati TFF haikutaja sababu hasa za kusimamishwa na kujiuzulu kwa viongozi hao lakini inadhaniwa kuwa sakata la mechi ya mahasimu wa soka Simba na Yanga ndilo lililochangia.
Mechi baina ya mahasimu hao wa soka nchini imeingia katika sintofahamu baada ya kuahirishwa mara mbili huku mjadala mkubwa ukiibuka miongoni mwa mashabiki wa klabu hizo mbili.
Katika mjadala huo baadhi ya mashabiki waliwalaumu viongozi wa TPLB kuwa ndio waliochangia kuahirishwa kwa mechi hiyo.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Machi 8 lakini iliahirishwa kwa kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama na kupangwa kuchezwa Juni 15, tarehe ambayo ilizidisha mjadala huku Yanga wakishikilia msimamo wa kutocheza.
Hatimaye mechi hiyo iliahirishwa kwa mara nyingine na sasa imepangwa kuchezwa Juni 25, uamuzi ambao pia umeanza kulalamikiwa na kupingwa na mashabiki wanaoaminika kuwa ni wa Simba.
Soka Kasongo asimamishwa TPLB, Mnguto ajiuzulu
Kasongo asimamishwa TPLB, Mnguto ajiuzulu
Read also
