Paris, Ufaransa
Kiungo wa zamani wa Man United, Paul Pogba inadaiwa yuko mbioni kujiunga na klabu ya Monaco ya Ufaransa ikiwa takriban miaka miwili imepita tangu aanze kutumikia adhabu ya kufungiwa kucheza soka.
Habari za ndani kutoka klabu ya Monaco zinaeleza kuwa mazungumzo ya awali baina ya Pogba na mabosi wa timu hiyo ya Ligi Kuu Ufaransa maarufu Ligi 1 yameanza.
Pogba, 32, kwa kipindi kirefu hajacheza soka la ushindani tangu afungiwe miaka minne na mamlaka za kisheria nchini Italia, adhabu aliyopewa Septemba, 2023 baada ya kubainika kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Adhabu ya mchezaji huyo hata hivyo baadaye ilipunguzwa na kuwa ya miezi 18 baada ya kukata rufaa lakini tayari klabu aliyokuwa akiichezea ya Juventus ilikubaliana naye kusitisha mkataba wake.
Tangu wakati huo hadi sasa, Pogba amekuwa nje ya soka la ushindani lakini sasa nyota huyo aliyekuwa katika kikosi cha Ufaransa kilichobeba taji la dunia mwaka 2018 yuko mbioni kujiunga na Monaco akiwa mchezaji huru.
Awali kulikuwa na habari kwamba mchezaji huyo alikuwa akiwindwa na klabu moja ya Saudi Arabia na matarajio ni kwamba angekuwamo kwenye michuano ya Fifa ya Klabu ya Dunia inayotarajia kuanza Jumapili hii nchini Marekani.
Monaco hata hivyo inatajwa kuwa na nia ya dhati ya kumsajili kiungo huyo ambaye alikuwa akitajwa kuwa miongoni mwa viungo bora wa soka kutoka Ufaransa kabla ya kukumbwa na kadhia ya madawa ya kuongeza nguvu.
Kimataifa Pogba kuibukia Monaco
Pogba kuibukia Monaco
Read also
