Na Hassan Kingu
Nimeikumbuka kauli ya kocha na beki wa zamani wa Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Tanzania au Taifa Stars, Mecky Maxime aliposema soka linaongozwa na wajinga wajinga.
Awali nilimpuuza lakini sasa nafikiria mara mbili mbili na kujiuliza kama nilikuwa sahihi kumpuuza au nilihitaji kutafakari kwa kina kuhusu kauli ile?
Kwa kinachoendelea katika soka letu nabaki najiuliza zaidi, je kwa kauli ile Maxime alikuwa sahihi au aliitoa tu katika mazingira ya hasira kutokana na mambo yanayowakuta makocha Tanzania?
Kinachoendelea baina ya Yanga, TFF na Simba kinanifanya nizidi kufikiri na kutafakari kwa mapana kama Maxime alikuwa sahihi au la?
Nikianzia Machi 8 mwaka huu, naliangalia tukio siku moja kabla kwa timu ya Simba kuzuiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi kabla ya mechi yao na Yanga, mazoezi ambayo ni utaratibu ulio rasmi na unatambulika hata na sisi tusio viongozi, nazidi kutafakari kwamba je tukio hili nalo si sehemu ya ule ujinga ujinga uliosemwa na Maxime?
Baada ya hapo hisia zinanipeleka katika tukio la kuahirishwa mechi yenyewe, tena kuahirishwa siku ya mechi, saa kadhaa kabla ya mechi, je hili nalo ni sehemu ya ule ujinga ujinga uliozungumzwa na Maxime au la?
Baada ya hapo najiuliza kuhusu tukio la kugomea mechi, nautafuta uharamu na uhalali wake, nakosa jibu lakini sichoki kutafakari na kujifikirisha mwisho wa yote nabaki najiuliza kama huu nao ni sehemu ya ule ujinga ujinga au la?
Sakata la kuahirishwa kwa mechi ya Yanga na Simba na kupangiwa tarehe nyingine yaani Juni 15 limeibua mgomo, huyu anataka mechi huyu hataki, natafakari vijembe na malumbano yanayoendelea hasa mitandaoni na swali langu linabaki lile lile je huu nao ni sehemu ya ujinga ujinga ulioanzia kwa viongozi?
Nawataja viongozi kwa sababu yote haya yanayoendelea yametokana na viongozi, watu ambao wamepewa dhamana ya kuongoza soka letu, mchezo unaopendwa na wengi lakini bahati mbaya sana Maxime amenifikirisha kwamba wengi wao ni wajinga wajinga na mwisho wa yote nabaki na swali lile lile, je ni kweli soka linaongozwa na wajinga wajinga?
Hadi sasa mashabiki wa soka wapo njia panda, mechi kubwa ya Yanga na Simba haijulikani kama ipo au haipo, je ni kweli kwamba mashabiki wamewekwa njia panda kwa sababu viongozi wenye dhamana ni wajinga wajinga?
Si katika sakata hili la mechi ya Yanga na Simba bali yapo mambo mengi ya kwenye soka letu yananifikirisha kuhusu suala zima la ujinga ujinga, kuanzia kwa maamuzi ya matukio mbalimbali yanayojitokeza, waamuzi na uchezeshaji wao, vyote hivi nikivichambua swali la ujinga ujinga linanijia.
Natafakari kuhusu usajili, mchezaji anasajiliwa kutoka nje ya nchi tena kwa bei mbaya lakini akiingia uwanjani huoni utofauti anaoleta katika timu, hapo hapo najiuliza kwamba mchezaji huyu si zao la kiongozi mmoja mjinga mjinga aliyemsema Maxime?
Dhana ya wajinga wajinga hainitoki kila ninapojaribu kuachana nayo, namuangalia tena mchezaji huyu huyu aliyesajiliwa kutoka nje ya mipaka ya Tanzania kwa bei mbaya lakini hana ubora na mwishowe anaishia kusugua benchi.
Mchezaji huyu anasaini mkataba ulio rasmi na unaotambulika kisheria halafu anaachwa kienyeji, anakwenda kulalamika kwenye mamlaka husika analipwa fedha nyingi na klabu, je huo nao si ule ujinga ujinga wa kiongozi mmoja mjinga mjinga aliyemzungumzia Maxime?
Sijachoka kuwaza kuhusu ujinga ujinga aliousema Maxime kwani hata hili sakata la pesa lililobuka hivi majuzi nalo kila nikilitafakari swali la ujinga ujinga au viongozi wajinga wajinga linanijia.
Nimefikia hitimisho la kuja na dhana kwamba huenda kuna wajinga wajinga wanaodhani kila mtu ni mjinga mjinga kiasi kwamba hata masuala ya pesa nayo yanaibua mjadala unaotoa kila dalili za kupelekana kwenye ujinga ujinga.
Imefikia hatua tunataka kudanganyana kwamba namba nazo zinaweza kuongopa kwamba 50 isomeke 70 na 70 isomeke 50, hili haliwezekani lakini kwa nini limeibuka, na je si kweli kwamba kuna ujinga ujinga mahali?
Kajisemea Bob Marley katika moja ya nyimbo zake ‘You can fool some people sometime but you cant fool all the people all the time’ yaani unaweza kuwadanganya/kuwapumbaza watu fulani kwa wakati fulani lakini huwezi kuwapumbaza/kuwadanganya watu wote kwa wakati wote.’
Huenda sakata linaloendelea sasa ni ishara kwamba tunakaribia kuelewana kwamba mwisho wa wajinga wajinga unakaribia.
Makala Je ni kweli soka linaongozwa na wajinga wajinga?
Je ni kweli soka linaongozwa na wajinga wajinga?
Read also
