Na mwandishi wetu
Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa wameingia katika vita ya kuumbuana, ni mfano wa ile hadithi ya wewe mwaga ugali na mimi nimwage mboga, ndicho kinachoendelea.
Jana Jumatatu Juni 9, 2025 Yanga walianza kutoa siri ambayo wadau wengi wa soka nchini walikuwa hawaifahamu kwamba klabu hiyo haikulipwa mgao wake wa ushindi wa michuano ya Kombe la Shirikisho CRDB.
Katika madai hayo, Yanga kupitia ofisa habari wao wameeleza kuwa wanaidai TFF Sh milioni 200 ambazo ni zawadi ya ushindi wa michuano hiyo.
TFF leo Jumanne imejibu madai hayo katika taarifa iliyosainiwa na ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo ambaye amekana kuwapo madai hayo.
Ndimbo katika taarifa hiyo kwanza amekiri kuwa Benki ya CRDB ni wadhamini wa mashindano hayo na akaisafisha benki huyo kwa kusema kwamba imetekeleza kila kitu katika mkataba wa udhamini huo.
Alieleza kwamba katika msimu wa 2023-24 benki hiyo ililipa fedha zote za kimkataba ambazo ni Sh milioni 255 kwa ajili ya uendeshaji wa mashindano hayo.
Sambamba na ufafanuzi huo Ndimbo pia alizungumzia habari za deni ambalo TFF inadaiwa na Yanga akaeleza kuwa ni TFF ndio wanaoidai Yanga.

Alifafanua kuwa Yanga waliomba kwa barua wakitaka fedha zao za zawadi katika mashindano mbalimbali zikatwe kulipia malipo wanayotakiwa kulipa kwa TFF zikiwamo ada za wachezaji wa kigeni.
TFF pia imeitaka klabu ya Yanga itume mtaalamu wao wa fedha katika ofisi za shirikisho hilo kesho Jumatano saa nne asubuhi ili kuhakiki deni la klabu hiyo akiwa na vielelezo vyote.
Baada ya TFF kutoa taarifa hiyo, Yanga nao muda mchache baadaye walitoa taarifa wakidai kuwa hawajawahi kulipwa zawadi ya ushindi wa michuano ya CRDB kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia msimu wa 2021-22.
Yanga wamedai kuwa hakuna uthibitisho wowote wa kimaandishi kuthibitisha kwamba TFF wamewahi kumlipa bingwa wa mashindano hayo kwa misimu mitatu mfululizo.
Klabu hiyo imewataka TFF wawalipe fedha zao za ushindi wa michuano hiyo kwa msimu wa 2023-24 ili waweze kucheza mchezo wa fainali ya michuano hiyo msimu wa 2024-25, mchezo ambao umepangwa kuchezwa Juni 28 mwaka huu.
Watu wa hesabu wanasema namba huwa haziongopi, je namba zitamaliza tatizo hapo kesho pande mbili zitakapokutana au itakuwa muendelezo wa kumwaga ugali na mboga.
