Warsaw, Poland
Mshambuliaji Robert Lewandowski amemshutumu kocha wa timu ya taifa ya Poland kwa kumsaliti baada ya kumvua unahodha na mchezaji huyo kuamua kuachana na timu ya taifa.
Kocha wa timu ya taifa ya Poland, Michal Probierz alifanya uamuzi wa kumvua unahodha wa timu ya taifa mshambuliaji huyo wa Barca na nafasi hiyo kumpa Piotr Zielinski.
“Kocha amemuarifu Robert Lewandowski, timu yote na maofisa wa timu hiyo kuhusu uamuzi alioifikia,” ilieleza taarifa ya Shirikisho la Soka Poland.
Dakika zipatazo 40 baada ya tangazo hilo, Lewandowski alitumia mitandao ya kijamii kutangaza kwamba anaacha kuichezea timu hiyo kama itaendelea kuwa chini ya Probierz.
“Kwa kuzingatia mazingira na kukosekana kuaminiwa na kocha wa timu ya Poland, nimeamua kujiweka kando katika kuichezea timu ya taifa ya Poland kama kocha wa timu ataendelea kuwa huyo huyo,” alisema Lewandowski.
Lewandowski licha ya kutoa msimamo huo lakini pia alisisitiza kwamba anaamini atapata nafrasi ya kuichezea timu hiyo kwa mara nyingine kwa ajili ya mashabiki bora duniani.
Lewandowski alisema kwamba aliarifiwa uamuzi wa kuvuliwa unahodha usiku kwa njia ya simu wakati akiwaandaa watoto wake kwenda kulala.
“Nilipata taarifa ya simu kutoka kwa kocha MichaÅ‚ Probierz kwamba ameamua kunivua unahodha, sikuwa nimejiandaa kwa namna yoyote, nilikuwa katika kuwaandaa watoto kwa ajili ya kulala,” alisema.
Alisema kwamba hakuwa hata na muda wa kuiarifu familia yake au kuzungumza na mtu yeyote kuhusu unahodha wake kwa sababu muda mfupi baadaye taarifa ilionekana kupitia mtandao.
Lewandoski, 36, alifafanua kuwa licha ya kukutana na Probierz baada ya mechi ya Ijumaa lakini hakuonesha dalili zozote kwamba alikuwa na mpango wa kumvua unahodha.
