Na Hassan Kingu
Baada ya Simba kulalamika kuzuiwa kuingia uwanjani kufanya mazoezi kabla ya mechi yao na Yanga iliyokuwa ichezwe Machi 8, 2025, nilijiaminisha kwamba Yanga itaadhiwa.
Niliiona Yanga imefanya jambo la hovyo, niliiona Yanga inahusika moja kwa moja na jambo hilo na isingeweza kukwepa lawama za uhusika wa tukio hilo kwa namna yoyote ile.
Nilipuuzia hoja zote za mitandaoni kwamba walioizuia Simba hawakuwa Yanga, bali niliona mbinu iliyotumika kwa sababu wanazozijua wenyewe Yanga kuwazuia Simba wasifanye mazoezi.
Nilijiaminisha kwamba kinachofuata ni Yanga kuadhibiwa kwa kiongozi au viongozi kupewa adhabu, klabu kutozwa faini au adhabu yoyote nyingine ambayo mamlaka za soka zingeamini inatosha kuwapa Yanga kwa mujibu wa kanuni.
Katika hilo sikuwa na shaka yoyote na hata Simba walipotoa tangazo lao la kususia mechi hiyo nilijiaminisha kwamba hawakuwa na haki hiyo, badala yake hisia zangu ziliniambia kwamba ilikuwa ni mikakati yao ya kuitingisha Yanga au mamlaka za soka.
Hadi hapo nilichokuwa nasubiri ni rungu la bodi ya ligi kwa klabu au viongozi wa Yanga lakini kinyume na matarajio hayo nilikutana na taarifa ya bodi ya ligi kuahirisha mechi hiyo.
Hili lilinishtua kidogo na kubaki najiuliza kulikoni bodi kuahirisha au kuifuta mechi kwa ghafla namna hiyo wakati mkosaji angeweza kuadhibiwa kwa kosa alilofanya.
Uamuzi wa bodi ya ligi ulinishangaza na nilijua kwamba japo bodi ndiyo yenye mamlaka ya kubadili ratiba za mechi lakini uamuzi wao kwa mechi ya Yanga dhidi ya Simba au Dabi ulikuwa na walakini na sikushangaa Yanga walipoanza kuja na masharti na kutangaza hawatacheza mechi hiyo.
Hadi sasa imepita miezi mitatu, bodi imetangaza mechi hiyo kuchezwa Juni 15 lakini msimamo wa Yanga umebaki ule ule kwamba hawatacheza.
Kuna hoja iliyotajwa katika taarifa ya bodi kuahirisha mechi hiyo kuhusu suala la usalama na kwamba baadhi ya matukio kwa mujibu wa ripoti ya ofisa usalama yalihitaji uchunguzi na hivyo wakaona ni vyema mechi kuahirishwa.
Umetimia mwezi wa tatu lakini bodi bado haijaweka wazi kuhusu suala hilo la usalama kwamba lilichangia vipi kuahirishwa kwa mechi au tatizo hilo la usalama lilikuwa katika namna gani.
Ni kweli kwamba hofu ya kiusalama ni sababu tosha ya kuahirishwa kwa mechi au tukio lolote lenye mkusanyiko wa watu wengi lakini ni vyema bodi ikaliweka wazi jambo hilo au ikaiweka wazi ripoti ya usalama au uchunguzi uliofanyika.

Kutofanyika yote hayo kunawafanya Yanga waamini kwamba kuahirishwa kwa mechi yao dhidi ya Simba kuna walakini, na hapo ndipo mashabiki na wadau wa soka wanapolazimika kuibuka na fikra au mitazamo mbalimbali inayojadiliwa mitandaoni.
Fikra mojawapo ni bodi kuwa na watu wa Simba wanaolinda maslahi ya Simba na wanataka timu hiyo itwae ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Hapo hapo kuna fikra nyingine za imani za kishirikina kwamba kuna watu walichungulia kwenye matunguri wakajiridhisha kwamba siku hiyo haikuwa nzuri kwa Simba na zikafanyika mbinu kulazimisha mechi iahirishwe.
Fikra nyingine ni kuhusu kikosi cha Simba wakati huo, mabeki Shomari Kapombe na Che Malone pamoja na kipa Musa Camara walikuwa majeruhi.
Kuumia kwa wachezaji hao wakati wa mechi muhimu dhidi ya Yanga ilikuwa hatari kwa Simba hivyo likatengenezwa tukio kwa kuwaingiza Yanga mtegoni nao wakaingia kwa kuwawekea vikwazo Simba wasifanye mazoezi, bodi ikapata sababu ya kuahirisha mechi.
Fikra nyingine zimeibuka kutokana na kauli za Rais wa TFF, Walace Karia, kitendo chake cha kulizungumzia suala hili kinatafsiriwa kuwa anaulinda uamuzi uliofikiwa na bodi wa kuahirisha mechi.
Kwa kuwa TFF imeipa bodi mamlaka ya usimamizi wa ligi, Karia alitakiwa kuacha mamlaka yake ilifanyie kazi jambo hilo yeye awe mtu wa mwisho kuzungumza au kutoa maamuzi, hapo sauti yake ingeheshimika lakini kwa sasa sijui atasema nini Yanga wamuelewe.
Mkwamo Yanga
Kwa hali ilipofika hapa tunaweza kusema kwamba Yanga imekwama mbele ya mamlaka za soka, kuanzia Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) pamoja na mahakama za ndani lakini hoja zao zina nguvu na ndicho kitu wanachojivunia.
CAS imewarudisha kwenye mamlaka za ndani za soka kwa kuamini kwamba kuna hoja au jambo ambalo linajadilika na linaweza kumalizwa na mamlaka za ndani.
Yanga hawana imani na mamlaka hizo na wana kila sababu ya kuwa na msimamo huo hasa inapofikia hatua kwa Rais wa TFF kuonesha tayari ana upande.
Na ndio maana msimamo wa Yanga umebaki kuwa ule ule wa hatuchezi, kabla ya kikao cha viongozi wa Yanga na bodi ya ligi msimamo ulikuwa huo na hata baada ya kikao hicho msimamo umebaki huo huo, ni msimamo uliozalishwa na maamuzi ya bodi, maamuzi ambayo yameiweka dabi njia panda.
