London, England
Kiungo wa zamani wa Man United, David Beckham (pichani) amesema kwamba amesikitishwa na kukatishwa tamaa na tabia za wachezaji wa timu hiyo wakati wakiwa katika ziara yao barani Asia.
Beckham ambaye alitamba na timu hiyo miaka ya 1990 alisema kwamba kuna mambo mengi yaliyokuwa yakifanywa na wachezaji hao ambayo hayakubaliki.
Winga wa timu hiyo, Amad Diallo alitoa ishara ya kidole cha kati mbele ya mashabiki wakati timu ikiwa katika hoteli moja mjini Kuala Lumpur, Malaysia akidai kwamba mama yake alitusiwa na hivyo hajutii alichokifanya.
Ijumaa iliyopita kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na picha iliyomuonesha winga wa timu hiyo, Alejandro Garnacho akiwa katika mzozo na shabiki ambaye inadaiwa alikuwa akimrekodi.
Man United ikiwa katika ziara hiyo ya Asia ilianza kwa kucheza chini ya kiwango mechi yake dhidi ya ASEAN All-Stars na kufungwa bao 1-0 kabla ya kubadili kibao na kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Hong Kong.
“Tunaelewa inamaanisha nini kuichezea Manchester United, tunaelewa nembo hii inamanisha nini, kila tulipokwenda iwe Ulaya au Asia, tuliheshimu mashabiki, tuliheshimu ukweli kwamba wametoka walipotoka na kulipa pesa kutuona sisi, kupiga picha nasi, kusaini vitabu nasi, ni lazima kuheshimu hilo,” alisema Beckham.
Beckham ambaye pia alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya England, mbali na Man United ambayo aliisaidia kubeba mataji kadhaa likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia aliwahi kuichezea Real Madrid.
