Cairo, Misri
Pyramids FC ya Misri imeweka rekodi kwa kulibeba kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini,
Ushindi huo uliopatikana Jumamosi hii usiku kwenye dimba la Air Force mjini Cairo, Misri umekuja baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi yao ya kwanza iliyopigwa mjini Pretoria, Afrika Kusini.
Kwa taji hilo, Pyramids sasa inaingia katika orodha ya wababe wengine wa soka nchini Misri yaani timu za Al Ahly, Zamalek na Ismailia ambazo ni timu pekee za Misri zenye rekodi ya kubeba taji la michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Afrika.
Kwa Afrika hakuna nchi ambayo timu zake nne zimefanikiwa kubeba taji la michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kudhaminiwa na Kampuni ya Total Energies.
Pyramids ikiwa mbele ya mashabiki wake ilianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya 27 lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga ya Tanzania, Fiston Mayele.
Kwa Mayele hilo ni bao lake la tisa katika michuano hiyo jambo ambalo linazidi kumpa hadhi mshambuliaji huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili, Pyramids waliongeza bao la pili mfungaji akiwa ni beki Ahmed Samy aliyeruka juu na kuiwahi krosi ya Mohamed Chibi na kuujaza mpira wavuni kwa kichwa.
Sundowns licha ya kuwa nyuma kwa mabao mawili, walionesha utulivu ambao hatimaye uliwalipa katika dakika ya 75 walipopata bao pekee la kufutia machozi lililofungwa na Iqram Rayners.
Katika dakika 10 za nyongeza, Sundowns waliendelea kuonesha utulivu huku wakisaka bao la kusawazisha lakini safu imara ya ulinzi ya Pyramids ikiongozwa na kipa Ahmed El Shenawy ilikuwa kikwazo.
Ushindi huo unakuwa jambo kubwa kwa Pyramids, klabu ambayo imeanzisha takriban miaka 10 iliyopita, ushindi ambao pia umeifanya timu hiyo iendeleze ubabe wa timu za Misri katika Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo baada ya Ahly kubeba taji hilo mwaka 2023 na 2024.
Kimataifa Pyramids wafalme Ligi ya Mabingwa Afrika
Pyramids wafalme Ligi ya Mabingwa Afrika
Related posts
Read also
