Liverpool, England
Nahodha wa timu ya Liverpool, Virgil van Dijk (pichani) anawaombea mashabiki wa Liverpool wapone haraka baada ya kugongwa na gari wakati wa maandamano ya kushangilia taji la Ligi Kuu England (EPL).
Watu wapatao 50 wamejeruhiwa wakiwamo watoto wanne baada ya gari moja kuvamia kundi la mashabiki hao waliokuwa wakisherehekea taji hilo katikati ya jiji la Livepool jana Jumatatu.
Mtu mmoja ambaye umri wake unatajwa kufikia miaka 53 amekamatwa akihusishwa na tukio hilo ambalo limeendelea kuwa mjadala.
Habari zaidi zinadai kwamba miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo, wanne kati yao hali zao ni mbaya.
“Fikra zangu na maombi yangu yapo kwa kila mmoja aliyeumizwa, nawaombea wapone haraka wote waliopata ajali, tuko pamoja nanyi,” alisema Van Dijk.
Naye kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp pia alisema kwamba wapo pamoja na wote waliopata ajali na madhara mengine kutokana na tukio hilo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Liverpool ipo pamoja na waliojeruhiwa na nchi yote ipo pamoja nao.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba maelfu ya mashabiki wa Liverpool walikuwa kwenye maandamano ya kufurahia ushindi wa taji la EPL msimu wa 2024-25 kabla ya gari moja kuvamia maandamano hayo na kuwagonga baadhi yao.
Awali polisi waliweka kizuizi katika mitaa ambayo mashabiki hao walipita lakini dereva wa gari hilo alipuuza na kutumia njia hiyo ndipo alipowagonga mashabiki hao.
Taarifa ya polisi baadaye ilieleza kuwa tukio hilo hawajalichukulia kama la kigaidi ingawa hawakuweka wazi nini hasa sababu ya mtu huyo kupuuzia katazo la polisi na hatimaye kuwagonga mashabiki.
