Madrid, Hispania
Kocha Xabi Alonso ametangaza kuanza kwa zama mpya mara baada ya kutambulishwa rasmi kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya Real Madrid ya Hispania.
Alonso, 43, jana Jumapili alisaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo ambayo pia amewahi kuichezea, anachukua nafasi iliyoachwa na Carlo Ancelotti ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil.
Real Madrid haikuwa vizuri msimu huu ikipoteza taji la La Liga mbele ya mahasimu wao Barcelona sambamba na mataji ya Copa del Rey na Supercopa na ikatolewa na Arsenal katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza leo Jumatatu Mei 26, 2025 kwenye uwanja wa mazoezi wa Real Madrid wa Valdebebas akiwa na rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, Alonso alisema huu ni mwanzo wa zama mpya.
Alisema kwamba mashabiki Real Madrid wanafurahia kuanza kwa zama mpya, kukua kwa timu na kuifanya historia ya klabu ya Real Madrid iwe kubwa zaidi.
“Ni siku ya kipekee, ni siku ambayo itabaki katika kumbukumbu kwenye kalenda yangu kwa maisha yote, nina furaha kuwa hapa, mahali ambapo najiona nipo nyumbani,” alisema Alonso.
Alonso ambaye msimu wa 2023-24 akiwa kocha Bayer Leverkusen aliiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga, pia alielezea uamuzi wake wa kurudi Real Madrid miaka 11 tangu aondoke akiwa mchezaji.
Alisema kwamba Real Madrid ina wachezaji wazuri, ni timu yenye fursa nyingi na yenye mambo mazuri kwa wakati huu na hata hapo baadaye.
Alisema mambo hayo yamempa sababu ya kurudi Real Madrid akiwa na nguvu na matumaini kwamba anaweza kufanikisha kilicho bora kutoka kwa wachezaji wote na kuijenga timu imara.
Alisema anaamini wanaweza kufanikisha mambo makubwa yenye hadhi ya Real Madrid na thamani ya mataji yote ya Ulaya mambo ambayo yamekuwa yakifaniikishwa na klabu hiyo kwa miaka mingi.
Alonso pia alimshukuru mtangulizi wake Ancelotti akisema kwamba alikuwa kocha wake, ni mtu mzuri na ana mchango mkubwa kwake na huenda bila yeye asingefika alipo sasa.
