Na mwandishi wetu
Matumaini ya Simba kucheza mechi yao ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa yamekwama na sasa ni rasmi mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Mechi hiyo ya pili itachezwa Mei 25, 2025 kwenye uwanja huo kwa maelekezo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jambo ambalo ni kinyume na matarajio ya Simba kutaka mechi hiyo ichezwe kwenye Uwanja wa Mkapa jijini, Dar es Salaam.
Taarifa ya klabu ya Simba iliyopatikana leo Jumatatu jioni hii Mei 19, 2025, imekiri kuwa licha ya juhudi za Serikali ya Tanzania na TFF kutaka mechi ichezwe Uwanja wa Mkapa lakini jambo hilo limeshindikana.
Simba katika taarifa hiyo imewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki.
KLabu hiyo imeahidi kesho Jumanne kufanya mkutano na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa taarifa rasmi na hatma ya mashabiki kuhusu mchezo huo muhimu.
Simba tayari imecheza mechi yake ya kwanza na Berkane ugenini nchini Morocco Jumamosi iliyopita na kulala kwa mabao 2-0.
Timu hiyo ilikuwa na shauku kubwa ya kuhakikisha mechi ya marudiano ambayo itamtoa bingwa wa michuano hiyo inachezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ambako timu hiyo ina mashabiki wengi.
Baada ya CAF kuzuia mechi hiyo kuchezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, mashabiki wa soka nchini wamekuwa wakilumbana kuhusu uamuzi huo huku wale wa Simba wakiamini mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkapa.
Uamuzi huo wa CAF umeacha maswali ambayo huenda yakajibiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari mojawapo ikiwa ni hatma ya mashabiki ambao tayari walinunua tiketi kwa imani kuwa mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa.
Uamuzi huo wa CAF umefikiwa kutokana na mapungufu mbalimbali ya kwenye Uwanja wa Mkapa ambayo licha ya kufanyiwa marekebisho lakini bado shirikisho hilo halijaweza kuridhia uwanja huo kutumika kwa mechi ya fainali ya michuano hiyo.
Kimataifa Rasmi, Simba, Berkane kukipiga New Amaan
Rasmi, Simba, Berkane kukipiga New Amaan
Read also
