Fenerbahce, Uturuki
Kocha wa Fenerbahce ya Uturuki, Jose Mourinho amekana kufanya mazungumzo na mabosi wa Shirikisho la Soka Ureno ili awe kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo.
Kumekuwapo habari katika siku za karibuni kwamba kocha huyo Mreno ataachana na klabu ya Fenerbahce mwishoni mwa msimu huu na kwenda kuchukua nafasi ya Roberto Martinez kwenye timu ya taifa ya Ureno.
Mourinho ambaye amewahi kuinoa timu ya FC Porto ya Ureno na kuiwezesha kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, majira ya kiangazi mwaka jana alisaini mkataba wa miaka miwili na Fenerbahce na bado hajasema lolote kama ataendelea na timu hiyo kwa msimu ujao.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo Mourinho hakulipinga badala yake alisema kitu pekee anachoweza kusema ni kukataa hoja ya kwamba amefanya vikao na mabosi wa Shirikisho la Soka Ureno kwa kuwa yeye ni mtu mtiifu.
“Wakati pekee ambao nilifanya mawasiliano ya moja kwa moja na klabu fulani niliwaarifu Fenerbahce, si sasa ilikuwa ni mwezi Januari, nilifanya kikao na klabu hiyo lakini sikukubali ofa yao na niliiarifu klabu yangu kabla hata ya kikao,” alisema Mourinho.
Rais wa klabu ya Fenerbahce, Ali Koc hivi karibuni alibainisha kwamba Mourinho alipata ofa ya Dola 40.6 milioni wakiwa katikati ya msimu ili aachane na Fenerbahce lakini aliikataa.
Mbali na timu za FC Porto na Fenerbahce, Mourinho pia amewahi kuzinoa timu za Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Man United na Tottenham Hotspur.