Leverkusen, Ujerumani
Kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso (pichani) amethibitisha kuwa anaachana na timu hiyo mwisho wa msimu huu huku akitajwa kujiunga na Real Madrid kumrithi Carlo Ancelotti.
Alonso ametangaza uamuzi wa kuachana na timu hiyo mbele ya waandishi wa habari lakini hakuwa tayari kutaja wapi anaelekea licha ya kwamba Real Madrid imekuwa ikiamini kuwa ndiye mtu sahihi wa kumrithi Ancelotti.
Akiwa Leverksen, Alonso ameweza kujipatia umaarufu hasa msimu wa 2023-24 akiiwezesha timu hiyo kumaliza mechi za ligi bila kupoteza hata mchezo mmoja hadi kubeba taji la ligi hiyo maarufu Bundesliga.
Kwa kipindi hicho tayari jina lake lilikuwa likitajwa Madrid ingawa mwenyewe aliweka wazi kwamba hakuwa tayari kuachana na timu hiyo wakati huo kwa kile alichodai kwamba kuna kazi alikuwa hajaimaliza.
Alipoulizwa na waandishi wa habari wapi anakwenda baada ya Leverkusen, Alonso alisema huu si wakati sahihi wa kuzungumza hilo lakini habari za ndani zinadai yuko katika hatua nzuri ya kukamilisha mipango ya kumrithi Ancelotti.
“Wiki hii mimi na klabu tumekubaliana kwamba nitakuwa na mechi mbili za mwisho katika nafasi ya kocha wa Bayer Leverkusen, ni suala la muda na sasa ni muda sahihi wa kutangaza hilo,” alisema Alonso.
Kwa upande wa Ancelotti ingawa mkataba wake Real Madrid unafikia mwisho mwaka 2026, klabu hiyo haina nia ya kuendelea naye kwa kinachoonekana kama tayari ameishiwa mbinu.
Huu umekuwa msimu mbaya kwa Ancelotti na Real Madrid licha ya kujipatia umaarufu baada ya kuiwezesha timu hiyo kubeba mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika miaka ya karibuni.
Baada ya kuachana na Real Madrid, Ancelotti anapewa nafasi kubwa ya kuwa Kocha wa timu ya taifa ya Brazil na tayari Shirikisho la Soka Brazil (CBF) limeweka wazi nia yao hiyo.
Kwa mujibu wa CBF baada ya kumalizana na Real Madrid, Ancelotti atakuwa na jukumu la kuiongoza timu ya Brazil katika mbio za kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
