Na Hassan Kingu
Baada ya shauri ya Yanga kugonga mwamba kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) uongozi wa klabu hiyo umetangaza kushikilia msimamo wao wa kutokuwa tayari kucheza mechi yao dhidi ya Simba.
Uamuzi huo uliofikiwa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo chini ya kiongozi wao mkuu Hersi Said umetangazwa rasmi leo Jumatatu, Mei 5, 2025 sababu kubwa ya kushikilia msimamo huo imetokana na kutokuwa na imani na mamlaka za soka nchini.
Yanga walikuwa wakipinga kuahirishwa kwa ghafla mechi yao dhidi ya Simba ambayo awali ilipangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu lakini Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliahirisha mechi hiyo saa chache kabla ya muda wa kuchezwa kufikia.
Bodi ya ligi ilitangaza sababu kadhaa za kuahirisha mechi hiyo zikiwamo za kiusalama jambo ambalo uongozi wa Yanga haukuliafiki na kuamua kulifikisja suala hilo CAS.
Awali Yanga walitaka wapewe pointi tatu baada ya Simba kutangaza kutocheza mechi hiyo sababu ikiwa kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mkapa siku moja kabla ya mechi lakini baada ya bodi ya ligi kuiahirisha ndipo Yanga walipokimbilia CAS.
Katika majibu yao ya hivi karibuni, CAS waliutaka uongozi wa Yanga kulifikisha suala hilo katika mamlaka za soka nchini kwanza ili uamuzi ufikiwe.
Maelekezo hayo ya CAS yameonekana kuwa magumu kwa Yanga kwa madai kwamba hawako tayari kulipeleka suala hilo kwenye mamlaka ambazo zinatenda dhulma.
“Kutokana na uonevu, uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo dhahiri kwa baadhi ya timu unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka Tanzania, uongozi wa Yanga hauna imani na haupo tayari kupeleka shauri hilo kwenye mamlaka ambazo zinatenda dhulma,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Yanga.
Katika taarifa hiyo wanayanga wote pia wamehimizwa kuipambania haki yao kivyovyote ili kukomesha dhulma na ukiukwaji mkubwa wa kanuni unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka.
