Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane amesema anajisikia raha kwa kufuta ukame wa vikombe baada ya timu yake kutwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga jana Jumapili.
Kane ambaye huu ni msimu wake wa pili na timu hiyo amekuwa na ukame wa mataji kwa kipindi kirefu lakini hatimaye jana Bayern walitawazwa rasmi mabingwa wa Bundesliga baada ya Bayer Leverkusen kutoka sare ya mabao 2-2 na Freiburg.
Wiki mbili zilizopita, Kane aliweka rekodi ya kipekee kwa kufikisha idadi ya mabao 60 katika mechi 60 za ligi akiwa na Bayern katika msimu wake wa pili.
Kane pia anajiandaa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo maarufu duniani katika misimu yake miwili ya kwanza.
Akizungumzia furaha ya kubeba taji la Bundesliga, Kane alisema kwamba si yeye tu bali ilikuwa siku ya kipekee kwa wachezaji, maofisa na kila mmoja ana furaha.
“Najiona mtu wa kipekee, nimekuwa nikisubiri kwa muda mrefu, ni dhahiri kwamba hili limetokana na juhudi, kujituma na najisikia furaha kushinda taji la kwanza katika maisha yangu ya soka,” alisema Kane.
Kane, mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur, hadi sasa amefunga jumla ya mabao 400 kwa klabu na timu yake ya taifa ya England.
Kwa upande mwingine Kane pia anashika nafasi ya pili kwa washambuliaji wenye mabao mengi katika Ligi Kuu England (EPL) akiwa ametanguliwa na Allan Shearer.
