London, England
Baada ya Arsenal kufungwa bao 1-0 na PSG katika nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta amesema kikosi chake kinatakiwa kufanya kitu cha kipekee ili kufuzu hatua ya fainali.
Arsenal ikiwa Emirates Jumanne iliyopita ilishindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani na kujikuta ikilala kwa bao hilo pekee lililopachikwa wavuni na Ousmane Dembele.
Kwa matokeo hayo, timu hiyo ya London sasa ina kazi ngumu ya kupindua meza timu hizo zitakaporudiana wiki ijayo ambapo PSG watakuwa nyumbani mjini Paris, mechi ambayo itatoa mshindi atakayecheza hatua ya fainali.
“Kama unataka kushinda kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa lazima ufanye kitu cha kipekee, tunakwenda kufanya hivyo na ni lazima tufanye kitu cha kipekee mjini Paris,” alisema Arteta.
PSG licha ya kuwa ugenini lakini ilitawala vyema mchezo huo katika dakika 20 za awali huku safu yao ya ulinzi ikifanikiwa kuyavuruga vyema mashambulizi ya Arsenal.
Arteta pamoja na timu yake kufungwa lakini alisema kwamba bado wana nafasi kubwa ya kufikia hatua ya fainali na nafasi hiyo itakuwa katika jiji la Paris.
“Tuna nafasi kubwa mno ya kufikia fainali, narudia tunachotakiwa ni kufanya kitu cha kipekee katika mashindano haya ili kuwa na haki ya kufikia fainali, na wakati wa kufanya hivyo itakuwa ni Paris,” alisema Arteta.
Arsenal mara ya mwisho kufikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa msimu wa 2005-06 lakini ilishindwa kutamba mbele ya Barcelona wakati PSG inasaka taji lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
