Na mwandishi wetu
Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi ametozwa faini ya Sh 500,000 kwa kufanya vurugu na kuwarushia chupa ya maji waamuzi wa mchezo wao na Singida BS ambao walifungwa bao 1-0.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kocha huyo alifanya kosa hilo mara baada ya mchezo huo kufikia tamati.
Kamati hiyo pia imezitoza faini ya Sh milioni moja kila moja timu za Tanzania Prisons, Tabora United na Fountain Gate kwa makosa mbalimbali katika mechi zao za hivi karibuni.
Prisons wakiwa wenyeji wa mechi yao na Kagera Sugar wamepewa adhabu hiyo kwa kosa la watoto waokota mipira kuficha na kuchelewesha kwa makusudi kurejesha mipira uwanjani.
Watoto hao inadaiwa kuanzia dakika ya 63 walianza kuchelewesha mipira hiyo na hadi inafika dakika ya 80 mpira mmoja tu ndio uliobaki uwanjani na hadi mechi inamalizika Prisons walitoka na ushindi wa bao 1-0.
Prisons pia walipewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kwa dakika 12 kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi yao na KMC, mechi ambayo KMC walishinda kwa mabao 3-2.
Kwa upande wa Tabora United wao wameadhibiwa kwa kosa la kukataa kuingia kwenye vyumba vya kuvalia wakati wa mechi yao na Pamba walioshinda kwa bao 1-0, kwa kile walichodai kuwa chumba hicho kilikuwa na harufu isiyo ya kawaida.
Baadaye kamishna na mratibu wa mchezo huo kwa kushirikiana na daktari baada ya kukagua chumba hicho ilibainika kuwa harufu hiyo ilikuwa ya sabuni iliyotumika kufanyia usafi.
Fountain Gate nao wameadhibiwa kwa kosa kama la Tabora, katika mechi yao na Pamba iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 lakini wao walikataa kuingia katika chumba cha kuvalia kwa madai kwamba kilikuwa na joto.
Rungu latua Championship
Kamati hiyo pia imemfungia mwezi mmoja na kumtoza faini ya Sh 300,000 meneja wa timu ya Mapinduzi FC, David Kinasa kwa kosa la kumtolea lugha chafu mwamuzi wa mchezo wao na Tunduru Korosho.
Meneja huyo pia alipewa kadi nyekundu katika mchezo huo wa Ligi ya Champioship ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Timu nyingine za Ligi ya Championship, Polisi Tanzania imepewa onyo na kamati hiyo kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi yao na Green Warriors, ambayo Polisi walishinda kwa mabao 3-2.
Timu ya Mbeya Kwanza nayo imepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne badala ya watano kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo wao na Kiluvya FC ambao Mbeya Kwanza walishinda kwa bao 1-0.
Nayo Tunduru Korosho imepewa onyo baada ya wawakilishi wake kushindwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi yao na Dar City iliyoisha kwa Dar City kupata ushindi wa mabao 3-0.
Soka Chupa ya maji yamponza kocha Azam
Chupa ya maji yamponza kocha Azam
Read also