Madrid, Hispania
Beki wa Real Madrid, Antonio Rudiger amefungiwa mechi sita baada ya kupewa kadi nyekundu katika mechi ya fainali ya Copa Del Rey dhidi ya Barcelona wakati mchezaji mwenzake, Jude Bellingham amefutiwa adhabu.
Rudiger, Bellingham na Lucas Vázquez ambaye pia alifungiwa mechi mbili wote walitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu katika dakika za nyongeza za mechi hiyo ambayo Real Madrid ililala kwa mabao 3-2.
Wachezaji hao wote walitolewa baada ya kuibuka tafrani sababu ikiwa ni kutokubaliana na maamuzi ya mwamuzi wa mechi hiyo, Ricardo Bengoetxea.
Katika taarifa yake Bengoetxea alisema kwamba Rudiger ambaye tayari kocha wake alikuwa amemfanyia mabadiliko, alitolewa katika dakika ya 120 kwa kurusha kitu kwenye eneo la wasimamizi.
Katika tukio hilo la Jumamosi iliyopita ambalo mwamuzi alilitafsiri kuwa ni kuonesha tabia ya ukorofi, Rudiger alijikuta akizuiwa na wachezaji wenzake na maofisa wa benchi la Real Madrid.
Vázquez ambaye kama ilivyokuwa kwa Rudiger naye alikuwa amefanyiwa mabadiliko, kosa lake lilikuwa ni kuingia eneo la kuchezea wakati akijaribu kupinga baadhi ya maamuzi ya Bengoetxea.
Kuhusu Bellingham yeye alipewa kadi nyekundu mara baada ya mchezo kumalizika kwa kosa la kuwazonga waamuzi hadi kuzuiwa na wenzake wakati akipinga baadhi ya maamuzi yao, kosa ambalo Bengoetxea pia alilitaja kuwa ni tabia za ukorofi.
Mapema wiki hii, kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Hispania ilitangaza kwamba Rudiger atatumikia adhabu ya kukosa mechi sita wakati Vazquez atatumikia adhabu ya kukosa mechi mbili.
Baadaye Rudiger alijirudi kwa tukio hilo na kutumia mitandao ya kijamii kuomba msamaha kwa kilichotokea wakati wa mechi hiyo.
“Hakika hakuna msamaha kwa tabia yangu, samahani sana kwa hilo, baada ya dakika 111 sikuweza tena kuisaidia timu yangu na kabla ya filimbi ya kumaliza mchezo nilifanya kosa, samahani kwa mara nyingine kwa waamuzi na kila mmoja aliyesikitishwa,” alisema Rudiger.
Kamati ya nidhamu hata hivyo haikukubaliana na hoja ya klabu ya Real Madrid kudai kuwa kitendo cha Rudiger kujutia kosa lake baadaye kizingatiwe kabla ya kutoa adhabu badala yake ilisisitiza kwamba taarifa za kwenye mitandao ya kijamii haziwezi kutumiwa kuwa ushahidi unaojitosheleza.
