Na mwandishi wetu
Steven Mukwala ameipendezesha Simba katika Ligi Kuu NBC baada ya kufunga mabao matatu (hat trick) na kuiwezesha timu yake kutoka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal Union.
Kwa matokeo hayo yaliyopatikana Jumamosi hii, Machi Mosi, 2025 kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Simba sasa imefikisha pointi 54 ikiendelea kusalia nafasi ya pili.
Mukwala alianza kuzitikisa nyavu za Coastal katika dakika ya 30 akiunganisha kwa shuti la mguu wa kulia pasi ya David Kameta.
Wenyeji Coastal walipambana kutaka kusawazisha bao lakini Mukwala kwa mara nyingine aliipatia Simba bao la pili muda mfupi kabla ya mapumziko akiitumia pasi ya Elly Mpanzu.
Mukwala alikamilisha bao la tatu katika dakika ya 56 safari hii akinufaika na makosa ya kipa wa Coastal, Chuma Ramadhan ambaye aliutema mpira uliopigwa na Mpanzu kabla ya kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.
Matokeo hayo yanaifanya Coastal kubaki nafasi ya tisa ikiwa na pointi 24 huku ikiwa na mwendelezo wa matokeo yasiyo ya kuvutia katika mechi tano zilizopita ambapo imeambulia sare na kufungwa mitatu.
Kwa upande wa Simba ambayo Jumamosi ijayo itacheza na mahasimu wao Yanga, pamoja na kupata ushindi huo dhidi ya Coastal lakini bado imeachwa na Yanga kwa pointi nne ingawa Yanga imecheza mechi moja zaidi ya Simba.
Mechi hiyo ambayo itakuwa ya mwisho kwa msimu huu wa ligi baina ya timu hizo mahasimu inatajwa na wadau wengi wa soka kuwa ndiyo yenye kutoa mwelekeo wa nani atavuna nini msimu huu.
Soka Mukwala atupia matatu Simba ikiilaza Coastal 3-0
Mukwala atupia matatu Simba ikiilaza Coastal 3-0
Read also
