Manchester, England
Mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford anatarajia kufanyiwa vipimo vya afya kwa lengo la kujiunga na klabu ya Aston Villa kwa mkopo wakati wowote kabla ya Jumatatu.
Kesho Jumatatu, Februari 3, 2025 ndiyo siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo na habari zinadai kwamba Aston Villa wapo katika hatua nzuri ya kukamilisha usajili huo.
Rashford, 27, amekuwa akipitia kipindi kigumu Man United chini ya kocha Ruben Amorim ambaye amekuwa akimuweka kando tangu Desemba 12 mwaka jana.
Mpango wa kupima afya kwa mchezaji huyo katika klabu ya Aston Villa ni habari njema kwake kwani siku chache zijazo huenda akayaanza maisha mapya ya soka chini ya kocha Unai Emery.
Katika kudhihirisha kwamba Amorim hamtaki Rashford, wiki iliyopita kocha huyo alisema ni afadhali ampe nafasi kwenye benchi la timu hiyo kocha wa makipa wa timu hiyo mwenye umri wa miaka 63 kwa sababu kwake Rashford si mwenye kujituma.
Jumatano iliyopita hata hivyo Amorim alinukuliwa akisema anaamini kikosi chake kinaweza kuwa bora wakiwa na Rashford lakini mchezaji huyo bado hajafikia kiwango na mahitaji ya timu.
“Jaribu kufikiri tunakuwa na kipaji cha Rashford katika timu yetu, itakuwa bora zaidi lakini ni lazima abadilike, kama atabadilika tutamkaribisha vizuri na tunamhitaji lakini kwa sasa lazima tuweke viwango, tunamsubiri,” alisema Amorim.
Aston Villa si timu ya kwanza kuhusishwa na mipango ya kumsajili mchezaji huyo, timu nyingine ni PSG, Barca pamoja na Napoli.
Rashford amekuwa na Man United tangu akiwa kijana mdogo wa miaka saba na amekuwa akipanda hatua kwa hatua ndani ya klabu hiyo hadi kufikia kikosi cha kwanza.
