Manchester, England
Hadithi iliyowahi kuvuma ya Erling Haaland kuhamia Real Madrid au Barcelona huenda haipo tena baada ya mshambuliaji huyo kusaini mkataba wa miaka tisa na nusu na klabu ya Man City.
Haaland amekuwa akihusishwa zaidi na mipango ya kujiunga na Real Madrid, alikuwa na mkataba Man City uliotakiwa kuishia mwaka 2027 kabla ya kuongeza na sasa mkataba huo utafikia mwisho mwaka 2034.
Wakati akihusishwa na mipango ya kuhamia Real Madrid, zilikwapo habari kwamba katika mkataba wake na Man City kulikuwa na kipengele kilichompa uhuru wa kuhama ingawa kocha wake Pep Guardiola alikanusha jambo hilo.
Man City walitangaza Ijumaa hii kuhusu Haaland kuongeza mkataba hadi mwaka 2034 lakini klabu hiyo haikuweka wazi maslahi ya mchezaji huyo ingawa inadaiwa ana maslahi manono.
Haaland, 24, ambaye alijiunga na Man City mwaka 2022 akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani anaingia katika rekodi ya wachezaji wa Ligi Kuu England (EPL) wenye mikataba mirefu.

Mchezaji mwingine wa EPL mwenye rekodi inayokaribia ya Haaland ni Cole Palmer ambaye Agosti mwaka jana alisaini mkataba wa miaka tisa na klabu ya Chelsea.
“Nina furaha hasa kwa kusaini mkataba wangu mpya na kuwa tayari kuangalia yajayo na kuendelea kuwa katika klabu hii kubwa,” alisema Haaland.
Kwa upande wake Pep alisema kwamba uamuzi wa Haaland kuongeza mkataba ni ishara ya kuwa na imani na timu hiyo.
Haaland ambaye amekuwa akidaiwa kuwindwa na Real Madrid na Barcelona huku Real Madrid ikitajwa zaidi, amejipatia mafanikio makubwa Man City na Ulaya kwa rekodi yake ya kuvutia katika ufungaji mabao.
