Munich, Ujerumani
Kipa wa zamani wa Arsenal, Jens Lehmann anadaiwa yuko mbioni kuupiga bei mjengo wake wa kifahari baada ya kuwapo habari za kutibuana na mkewe.
Lehman (pichani chini) ambaye pia amewahi kuwa kipa wa timu ya taifa ya Ujerumani, alikuwa katika kikosi cha Arsenal kilichobeba taji la Ligi Kuu England mwaka 2004 kikiwa chini ya kocha Arsene Wenger.
Chanzo kimoja cha habari kimeripoti kuwa kipa huyo amekuwa katika wakati mgumu na mkewe aitwaye Conny ambaye kwa sasa haishi katika mjengo huo.
Lehman mwenye umri wa miaka 55 na Conny mwenye umri wa miaka 52 walifunga ndoa mwaka 1999 lakini ndoa yao imepitia kipindi kigumu na kwa sasa Conny anadaiwa kuwa na mpenzi mwingine ambaye anatajwa kuwa ni kijana mdogo.
Habari zaidi zinadai kwamba kwa kipindi kirefu ndoa ya Lehman na Conny imekuwa katika misukosuko japo wamekuwa wakijitahidi kuonekana mbele ya umma kama kila kitu kipo sawa.
Tangu kuondoka kwa Conny, Lehman amekuwa akiishi peke yake na watoto wao wawili, pamoja na mtoto wa tatu ambaye ni wa Conny katika mahusiano yake ya awali.

Wakala mmoja wa serikali mjini Munich anadaiwa kutangaza mpango wa kupigwa bei kwa mjengo huo ambapo bei yake imetajwa kufikia Pauni 10.7 milioni.
Mjengo huo wa kifahari wenye vyumba sita, una kila kitu cha kwenye nyumba ya kifahari, likiwamo bwawa la kuogelea, sehemu ya mazoezi, sauna na unatazama Ziwa Starnberg la mjini Munich.
Lehmann amekuwa akiandamwa na tatizo la ulevi ambapo aliwahi kukamatwa na polisi mjini Municha kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kujikuta akinyang’anywa leseni.
Inadaiwa kwamba baadhi ya majirani wamefurahi kusikia habari za kuuzwa kwa mjengo huo kwa kile kinachodaiwa kwamba kipa huyo alikuwa kero mno kwao ikiwamo kugombana nao huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni ulevi uliopindukia.
Inadhaniwa kwamba tatizo la ulevi wa Lehman ni sababu mojawapo iliyomfanya Conny aondoke kwenye mjengo huo wa kifahari na kuanza mahusiano na mpenzi wake mpya.
